NDUGUYE AFISA IEBC ATOROKA

Asema amekuwa akitumiwa jumbe za vitisho akidai zinalenga dadaye na makamishna wenzake

Taifa Leo - - FRONT PAGE - Na JUSTUS WANGA

KAKAKE kamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Roselyn Akombe ametoroka nchini baada ya kupokea jumbe kadha

za vitisho zinazoaminika kulenga dadaye na makamishna wenzake.

Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 34, ambaye hatutamtaja jina kwa sababu za kiusalama, mkewe na wanawe watatu waliondoka nchini kupitia kituo cha mpakani cha Namanga mnamo Septemba 5.

Hii ni baada ya maisha yake kutishiwa na watu wasiojulikana katika kile kinachodhaniwa kuwa mpango wa kuwatisha makamishna wa tume hiyo, hasa wale wanaodhaniwa kuwa wakaidi.

“Aliondoka nchini wiki iliyopita alipozidiwa na vitisho,” Bi Akombe aliambia Taifa Jumapili kwenye mahojiano ya kipekee.

Bila kumlaumu mtu yeyote Dkt Akombe alishikilia kuwa vitisho vilivyoelekezwa kwa kakake vilinuiwa kumfikia yeye mwenyewe.

“Ni mtu anayeipenda nchi hii na kila mara amekuwa akipuuzilia mbali shinikizo za kumtaka afanye kazi ng’ambo. Nawajibikia masaibu yake... sio vizuri lakini nitafanya nini?” Akombe akasema kwa hofu.

Taifa Jumapili ilifahamishwa kwamba mwanaume huyo ambaye alikuwa mfanyakazi katika mojawapo ya wizara katika serikali kuu, hakutaka kupitia Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kutokana na sababu za kiusalama. Badala yake aliamua kusafiri kwa barabara hadi Namanga kabla ya kuvuka mpaka na kuingia Tanzania.

Alipita mataifa matano kabla ya kufika katika taifa ambako alilenga kupata hifadhi.

Dkt Akomba pia alisema anahofia maisha yake, akisema usalama wake haujawahi kutishiwa kama ilivyo sasa.

“Nimewahi kwenda Somalia, Yemen, Jordan, Iraq na hata Libya kufanya kazi ya kuchunguza hali ya kiusalama, lakini binafsi usalama wangu haujawahi kutishiwa kiasi hiki,” akasema bila kutoa ufafanuzi zaidi.

Kamishna huyo alikuwa akirejelea ziara za kikazi zilizomfikisha katika mataifa hayo, ambayo yamezongwa na utovu wa usalama, alipohudumu katika Idara ya Masuala ya Kisiasa katika Umoja wa Mataifa (UN).

Alishikilia cheo cha katibu msaidizi katika idara hiyo, kabla ya kupewa likizo ili ahudumu kama kamishna wa IEBC mapema mwaka huu.

Alipoulizwa iwapo amepiga kwa polisi kuhusu kisa hicho cha nduguye, alisema hajafanya hivyo lakini hakutoa sababu zozote zilizomfanya asiripoti.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.