Jinsi ilivyo vigumu kwa Jubilee kumng’oa Raila

JAMVI UK 11 - 15

Taifa Leo - - FRONT PAGE - Na CHARLES WASONGA

MAJUZI Rais Uhuru Kenyatta aliwashangaza wengi aliposema kuwa chama cha Jubilee kitatumia wingi wa wabunge wake kumng’oa mamlakani kiongozi wa upinzani Raila Odinga endapo atashinda urais katika marudio ya uchaguzi ulioratibiwa Oktoba 17.

Akihutubia ujumbe wa viongozi wa Ukambani waliomtembelea katika Ikulu ya Nairobi, Rais alieleza kuwa chama chake kina wabunge 220 katika bunge la kitaifa na kinahitaji wabunge 13 pekee kufikisha 233, idadi ya wabunge wanaohitajika, kikatiba, kufanikisha hatua kama hiyo.

“Tunajua Raila hatashinda. Lakini hata akishinda tutamtoa baada ya miezi miwili au mitatu kupitia bunge kwani tuna idadi tosha ya wabunge kufanya hivyo. Leo hii hata akichaguliwa atatawala Kenya namna gani?” Rais Kenyatta akauliza.

Lakini wadadisi wa masuala ya kisiasa na kisheria wanasema kuwa chama cha Jubilee kitakabiliwa na kibarua kigumu kumwondoa rais aliyemlakani chini ya Katiba ya sasa.

Isitoshe, wanasema mwenendo wa wanasiasa wa kubadili misimamo, kisiasa, kutokana na vishawishi kutoka Ikulu utahujumu nia, na mchakato mzima, wa kupitishwa kwa kura ya

kutokuwa na imani na rais katika mabunge yote mawili; bunge la kitaifa na seneti. Hali kama hiyo imeshuhudiwa nchini tangu kurejelewa kwa mfumo wa utawala wa vyama vingi mapema miaka ya ‘90.

Na huku wabunge wa Jubilee wakiunga mkono kauli ya Rais Kenyatta, wenzao wa muungano wa NASA wanataja wazo hilo kama “ndoto ya mchana na ithibati kuwa Rais Kenyatta alishindwa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8”.

Wakili Bob Mkangi analitaja wazo la Rais Kenyatta kama la kisiasa na ambalo haliwezi kutekelezwa kwa urahisi kwa mujibu wa katiba ya sasa.

“Utaratibu wa kumwondoa mamlakani Rais unafafanuliwa katika kipengee cha 145 cha Katiba. Japo suala la idadi ya wabunge ni muhimu katika mchakato wa kufanikishwa kwa hoja ya kumwondoa rais mamlakani, sharti pawepo ushahidi tosha kwamba rais huyo amevunja Katiba au amehusika katika uhalifu kwa mujibu wa sheria za humu nchini au za kimataifa,” anasema.

“Itakuwa vigumu kwa bunge la kitaifa na seneti kumpata rais na makosa kama hayo kwa kipindi cha miezi mitatu ndiposa hoja ya kumwondoa mamlakani iweze kupitishwa,” anasema Bw Mkangi ambaye ni wakili wa masuala ya kikatiba.

Kulingana na kipengee hicho, hoja ya kumwondoa mamlakani rais sharti iidhinishwe na thuluthi moja ya wabunge (yaani wabunge 116) kisha wabunge 233 waipitishe, (yaani thuluthi mbili ya wabunge 349).

Baada ya hatua hiyo, Spika wa Bunge la Kitaifa atawasilisha hoja hiyo kwa Bunge la Seneti. Bunge hilo litasikiza madai hayo kabla ya kuteua kamati ya maseneta 11 kuchunguza suala hilo kwa muda wa siku 10.

Kamati hiyo itawasilisha ripoti kuhusu iwapo madai dhidi ya rais yana mashiko au la.

Endapo, kamati hiyo itakubaliana sababu zilizotolewa kwenye hoja hiyo, kama ilivyopitishwa na bunge la kitaifa, ripoti hiyo itahitaji kupitishwa tena na angalau thuluthi mbili ya maseneta (maseneta 45 kati ya 67) kwenye kikao cha bunge lote.

Rais atakoma kuwa mamlakani ikiwa idadi hii ya wanachama wa Seneti watapitisha ripoti hiyo au asalie afisini ikiwa itaungwa mkono na maseneta wanaopungua 45.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Dismas Mokua anashilikia kuwa, katika muktadha wa siasa za Kenya, ni vigumu kumwondoa mamlakani rais kupitia hoja ya mabunge hayo mawili.

Kwenye mahojiano katika runinga moja ya humu nchini, Bw Mokua alisema tabia ya wanasiasa wa humu nchini ya kubadili misimamo yao ya kisiasa kutokana na ‘vishawishi’ kutoka Ikulu itasambaratisha mpango kama huo.

“Endapo Bw Odinga ataibuka mshindi katika marudio ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 17, kama ambavyo Rais Kenyatta alibashiri, bila shaka kibarua chake cha kwanza kitakuwa ‘kuwanunua’ wabunge wa Jubilee ili kujidhibiti mamlakani,” akasema.

“Kwanza atawalenga wabunge, na maseneta, waliochaguliwa kwa tiketi ya vyama vidogo pamoja na wale walioingia bungeni kama wagombeaji wa kibinafsi ambao kwa jumla ni takriban wabunge 50. Kisha, atawageukia wabunge kadhaa wa Jubilee, hasa wale wanaotoka nje ya ngome za Rais Kenyatta za Kati ya Kenya na Bonde la Ufa,” akaeleza Bw Mokua.

Kulingana na mchanganuzi huyo, Bw Odinga atahitaji takriban wabunge 80 zaidi kuweza kuendesha sera zake barabara endapo atashinda. Hii ni ikizingatiwa kuwa sasa NASA ina wabunge 139 katika bunge la kitaifa na maseneta 27 katika bunge la seneti.

“Akikumbatia mtindo huo, alivyofanya Rais Mstaafu Mwai Kibaki mnamo 2007, basi ataweza kuendesha sera na maongozi ya serikali yake ndani ya bunge pasina wasiwasi wowote,” alielezea Bw Mokua, kauli ambayo inaungwa mkono na wabunge kadhaa wa NASA.

Naye Profesa Edward Kisiang’ani anapuuzulia wazo la Rais Kenyatta, akisema lilinuiwa kuwakosesha matumaini wafuasi wa NASA ili wasione haja ya kumpigia kura.

“Rais Kenyatta anafahamu fika kwamba ilivyo sasa ni vigumu kumwondoa rais aliye mamlaka kupitia hoja bungeni. Yeye mwenyewe alifuata nyayo za mtangulizi wake (Bw Mwai Kibaki) na mlezi wake kisiasa, Mzee Daniel Moi, za kuwavutia wabunge wa upinzani upande wake ili kujidhiti,” anasema.

“Vivyo hivyo, Bw Odinga ataiga mfano ambao utahujumu uwezekana wa kupitishwa kwa hoja ya kumwondoa mamlakani,” Profesa Kisiang’ani anaongeza.

Aidha, anatoa mfano wa aliyekuwa Rais wa Amerika Barack Obama ambaye aliongoza kwa kipindi cha pili ilhali chama chake, Democrat, kilikuwa na viti vichache katika bunge la Congress na lile la Seneti.

Lakini kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa Benjamin Washiali anasema endapo Bw Odinga atashinda, Jubilee itatumia wingi wabunge wake bungeni kuyumbisha utawala wake kwani mrengo wa NASA una wabunge wachache.

V inara wa Nasa wakiongozwa na Raila Odinga washerehekea na wafuasi wao baada ya matokeo ya urais kufutiliwa mbali na Mahakama ya Juu mnamo Septemba 1, 2017.

Picha/jeff Angote

Waziri Mkuu wa zamani, Bw Raila Odinga awapungia wananchi mkono huku akiondoka katika Mahakama ya Juu, Nairobi mnamo Agosti 28, 2017 ambapo kesi ya kupinga matokeo ya kura za urais ilikuwa ikisikilizwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.