Jubilee yatema Shahbal, yampokeza Balala mikoba

Taifa Leo - - FRONT PAGE - Na DANIEL NYASSY

CHAMA cha Jubilee kimeamua kumpokonya mfanyabiashara Suleiman Shahbal jukumu la kuongoza kampeni za Rais Uhuru Kenyatta eneo la Pwani.

Badala yake, waziri wa Utalii Najib Balala sasa atachukua mikoba hiyo, ili kuhakikisha kuwa viongozi wote wa Jubilee eneo hilo wanakuwa na lengo moja.

Kwenye mkutano na Naibu wa Rais William Ruto katika ukumbi wa Wild Waters mjini Mombasa, wajumbe wa chama hicho walimkataa Bw Shahbal aliyewania ugavana na kushindwa na Bw Hassan Ali Joho.

Mambo yalikuwa mabaya kwa mfanyabiashara huyo, alipozomewa na wajumbe alipojaribu kuwahutubia, huku wakisema kuwa amejifanya mtu wa hadhi, na anayewagawanya wanachama.

Bw Balala alijaribu kumtetea Bw Shahbal lakini umati ukaendelea kumzomea na kumlazimisha kuketi.

Kwenye hotuba yake, Bw Ruto alikiri kwamba kampeni za Jubilee kabla ya uchaguzi wa Agosti 8 zilikumbwa na utata sababu ya maajenti.

“Kulikuwa na mvutano mkubwa wa kiongozi huyu kuleta maajenti hawa na mwingine kuleta watu wake,” alisema Bw Ruto na kutangaza mikakati kadhaa sasa.

“Safari hii kampeni zitaenda mashinani kiwango cha kituo cha kupigia kura hadi wodi,” alisema naibu wa Rais.

Alitangaza kwamba hakuna tena “wakubwa” kutoka makao makuu ya chama Nairobi kuenda mashinani na kuongoza kampeni hizo.

“Watu wenyewe mashinani waendeshe kampeni hizo, waunde kamati za nyanjani na kuendesha kazi hiyo wao wenyewe. Hatutaki tena ubosi (ukubwa),” alisema.

Mapema kabla ya hafla ya Wild Waters, Bw Shahbal alijipata pabaya baada ya viongozi wa chama hicho kumkataa.

Wakiongea kwenye mkutano katika afisi za kibinafsi za waziri Balala huko Mombasa, viongozi hao walisema kamwe hawatafanya kazi na Bw Shahbal.

Mmoja wa wale waliohudhuria mkutano huo wa kwanza alisema kwamba wanachama walimlaumu kwa kuwa kizingiti kikubwa kabla ya Agosti 8.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.