Jamii yajaa hofu baada ya mti wa Mugumo kuanguka

Taifa Leo - - FRONT PAGE - Na PETER MBURU

JAMII ya Agikuyu, imebabaika na kulazimika kuwaita wazee kuingilia kati kutatua hali, baada ya mti mkubwa wa ‘Mugumo’ ambao unaheshimiwa sana na jamii hiyo kuanguka Kaunti ya Nakuru.

Mti huo uliokuwa kwenye eneo la Uwanja wa Maonyesho ya Kilimo, ulianguka Jumatatu wiki jana, na kuharibu mali ya thamani kubwa.

Hata hivyo, wafanyakazi wa uwanja huo waliamua kuuacha ulipoanguka kwani kulingana na tamaduni za jamii ya Agikuyu, haukufaa kuguswa na yeyote kabla ya ‘kusafishwa’ na wazee wateule kwa njia ya kitamaduni.

Matambiko ya kuondoa laana kutoka kwa mti huo yaliongozwa na mzee Dominic Ngera ambaye ni naibu mfalme wa wazee wa Agikuyu aliyeteuliwa kuchukua wadhifa huo mwaka uliopita, kwenye sherehe ya kitamaduni iliyoandaliwa mjini Nyeri.

Hata hivyo, kulingana na mkuu wa kutoa kafara na mzee wa kuhifadhi tamaduni za jamii hiyo mzee Mathenge Wa Iregi, mti huo ulianguka kutokana na upweke kwani ulipokuwa haukuwa na ‘rafiki’ (kwa maana ya mti mwingine wa ‘Mugumo’ wa kuliwazana nao.

“Sababu mbili kuu za mti huo kuanguka ni kuwa ulikuwa na upweke kwani hakuna Mugumo mwingine karibu na pili kwa kawaida miti hiyo huwa haina mizizi halisi na hivyo huingiza udhaifu kadri inavyokua,” akasema mzee Iregi.

“Mti huo ni wa maana sana na unaitwa mti wa “kirema nditi” kwani ulikuwa umejitenga na miti mingine,” mzee akaongeza.

Mzee huyo alieleza kuwa aliwaamrisha wazee wenzake kuchinja mbuzi kisha kuchanganya damu yake na uchafu wa tumbo ‘tatha’ na kunyunyizia mti huo kutoka kwenye mizizi hadi juu.

“Utamaduni huo ulikuwa wa maana sana ili kuondoa laana kwa yeyote ambaye angeuguza, lakini baada ya kutakaswa watu walikuwa huru kuukatakata na kufanyiakazi zingine,” Mzee Iregi akaeleza.

Hata hivyo, alisema kuwa kuanguka kwa mti huo hakukuwa na uhusiano wowote na mizozo ya uongozi inayoshuhudiwa nchini.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.