Mipango jikoni ya kuzolea Uhuru kura zote milioni 4.4 za Mlima Kenya

Makundi yaapa kutumia rasilimali zao kupiga kampeni

Taifa Leo - - FRONT PAGE - Na JOSEPH WANGUI

MAKUNDI mbalimbali katika eneo la Mlima Kenya yameanza mikakati ya kuhakikisha kuwa Rais Uhuru Kenyatta anazoa kura zote 4.4 milioni za eneo hilo katika uchaguzi mpya wa Oktoba 17.

Wafanyabiashara wakiongozwa na Thuo Mathenge, Ephantus Thuku wa vuguvugu la Team Adonia kutoka Nairobi na muuzaji magari Wambugu Nyamu walisema wafanyabiasha katika eneo hilo watatumia rasilimali zao kuwahimiza wapigakura kujitokeza kwa wingi.

Akiongea baada ya kuhudhuria mkutano wa kwanza wa kupanga mikakati ya kampeni katika hoteli ya White Rhino mjini Nyeri, Bw Mathenge aliwataka viongozi wote wa eneo hilo waliochaguliwa kushiriki katika kampeni za kumpigia debe Rais Kenyatta.

Alisema wapigakura 4,457,392 walioko katika kaunti 10 za Mlima Kenya za; Isiolo, Tharaka Nithi, Embu, Laikipia, Meru, Nyandarua, Kirinyaga, Kiambu, Murang’a na Nyeri kwa jumla wanaweza kumweka Rais Kenyatta katika nafasi bora ya kuibuka mshindi.

“Tumeamua kutumia rasilimali zetu kufadhili kampeni za Rais na Naibu wake William Ruto kwani wanastahili kuongoza kwa kipindi cha pili kutokana na utendakazi wao mzuri. Wale walioshindwa katika uchaguzi wa Agosti 8 wameungana nasi,” akasema Bw Mathenge.

Aliongeza kuwa wafanyabishara watashirikiana kwa karibu na wanasiasa kuwashawishi wapigakura wajitokeze kwa wingi. Pia, akaeleza, watawahamasisha kuhusu miradi ya miundo msingi ambayo imetekelezwa na utawala wa Jubilee katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Akiwahutubia wanahabari, Bw Mathenge alisema kampeni hizo zinalenga kuhakikisha kuwa kujitokeza kwa wapigakura kunafikia kima cha asilimia 100.

Alisema mshindi katika uchaguzi ujao wa urais ataamuliwa kwa misingi ya kiwango cha wapigakura watakaoshiriki. “Kwa hivyo, siri ya ushindi wa Jubilee ni kuhakikisha kuwa kila mpigakura anajitokeza kupiga kura yake,” Bw Mathenge akasema.

Kauli yake iliungwa mkono na Bw Nyamu ambaye aliwataka viongozi waliochaguliwa kuunda au kufufua makundi ya kampeni katika maeneo yao, kuanzia kiwango cha wadi hadi kaunti.

“Tumegundua kuwa baada ya kuibuka washindi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8, baadhi ya viongozi walielekea Nairobi na kujituliza. Kazi kubwa iliyoko mbele yetu ni kura ya Oktoba 17 na sharti tuhakikishe kuwa watu wetu wamejitokeza wote,” akasema Bw Nyamu.

Kiongozi wa wanawake, Elizabeth Muthoni Wanjau alisema kundi hilo la wafanyabiashara limebuni makundi ya kampeni maeneo ya mashinani kuanzia ngazi ya vituo vya kupigia kura.

Kundi hilo pia liliitaka Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuanza mchakato wa kutoa mafunzo kwa wapigakura ili kupunguza idadi ya kura zitakazoharibika au kukataliwa.

“Mafunzo kwa wapigakura ni muhimu zaidi katika marudio ya uchaguzo wa urais,”mmoja wa mwanachama wa kundi hilo Wambugu Ndirangu alisema.

Picha/joseph Kanyi

Bw Githinji Kinyanjui (kushoto) akiwa na mfanyabiashara Thuo Matheke kwenye kampeni.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.