Marufuku yapingwa

Sonko ajipata motoni kwa kutangaza kuwa magari ya umma hayataruhusiwa kuingia jijini

Taifa Leo - - HABARI ZA KAUNTI - Na JOSEPH WANGUI

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko, amejipata motoni siku moja baada ya serikali yake kutangaza kuwa Magari ya Uchukuzi wa Umma (PSVS), hayataruhusiwa kuingia katikati mwa jiji kuanzia Jumatano ijayo.

Shirika moja la kutetea wateja linamtaka Gavana Sonko kusitisha mipango hadi pale serikali ya kaunti itaunda mfumo thabiti, mwafaka na nafuu wa kuvusha watu upande wa pili, vituo vya magari ya moshi na steji kadha za mabasi.

Katibu mkuu wa shirika la Consumer Federation of Kenya (Cofek), Bw Stephen Mutoro, alisema marufuku hiyo haifai wala haiwezi kudumishwa ikizingatiwa marufuku za awali hazijafua dafu.

“Nairobi inahitaji mpango mahususi wa trafiki pamoja na uwekezaji unaohitajika,” akasema Bw Mutoro.

Alitaja marufuku hiyo kama ubaguzi dhidi ya wasafiri wanaotumia magari ya umma na kusema ni rahisi sana kwa mtu yeyote kuipinga mahakamani kwa misingi ya Kifungu 27(4) cha Katiba.

Katibu mkuu huyo wa Cofek alimtaka Bw Sonko kusitisha utekelezaji wa marufuku hiyo kwa angalau miezi mitatu ili kuweka mbinu mbadala za usafiri na miundo msingi inayohitajika.

“Weka mipangilio mwafaka ya utekelezaji isiyoweza kuathiriwa na ufisadi, ya tekonolojia na pia wahudumu. Unda maeneo ya kutosha ya kuegesha magari na ya wananchi kujikinga dhidi ya hali ngumu ya anga katika steji mpya zitakazopendekezwa,” alishauri.

Vilevile, alimtaka gavana kuwahakikishia wananchi usalama katika steji hizo, na kupendekeza serikali ya kaunti kuhamasisha kwanza wananchi kuhusu marufuku hiyo.

Aidha, alisisitiza kuwa magari ya kibinafsi pia yanafaa kupigwa marufuku kuingia katikati mwa jiji akisema ni ambulansi pekee na magari ya kuzima moto yanafaa kuruhusiwa jijini.

Cofek inataka malori ya mizigo yasitumie barabara kuu ya Uhuru Highway na bidhaa zafaa kuingizwa jijini usiku tu.

“Pikipiki na baiskeli za kubeba abiria, almaarufu bodaboda, zilizoidhinishwa ziruhusiwe kuingia katikati mwa jiji. Vile vile, uchuuzi wa bidhaa unafaa kudhibitiwa kikamilifu,” aliongeza Bw Mutoro.

Alisema Cofek inaunga mkono juhudi za gavana kukabiliana na msongamano wa trafiki katika jiji kuu.

Kwenye tangazo hilo, serikali ya Kaunti ya Nairobi ilisema kuwa marufuku hiyo ilichapishwa katika gazeti rasmi la serikali la Mei 12, 2017, na serikali iliyopita ya Gavana Evans Kidero.

Ili kutolea maoni habari hii, nenda kwa swahilihub.com

Picha/ Maktaba

Magari ya Matatu yakiwa kwenye msongamano katika barabara ya Moi Avenue jijini Nairobi mnamo Mei, 12, 2017. Marufuku imetolewa na serikali ya kaunti magari ya uchukuzi wa umma yasiingie jijini kuanzia kesho.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.