Hasara hoteli 2 za kifahari zikiteketea

Taifa Leo - - HABARI ZA KAUNTI - PHILIP MUYANGA na AHMED MOHAMED

MALI ya thamani isiyojulikana iliteketea mnamo Ijumaa jioni baada ya hotel mbili za kifahari mjini Mombasa ziliposhika moto.

Baadhi ya sehemu za hoteli ya Indiana na Ziwa zilizoko eneo la Bamburi, zilianza kuteketea dakika chache kufikia saa mbili usiku huku moto huo ukisababisha hasara kubwa.

Wakati wa moto huo, hakuna majeruhi wowote walioripotiwa, swala ambalo mkuu wa polisi eneo la Kisauni Christopher Rotich alithibitisha.

Bw Rotich aliiambia Taifa Jumapili ya kuwa wageni katika hoteli hizo mbili walikuwa wameondolewa salama na chanzo cha moto huo hakikuwa kimejulikana.

Wazimamoto kutoka Kaunti ya Mombasa wallifika eneo la moto dakika chache baada ya kuarifiwa na waliweza kuukabili wakisaidia na wenyeji.

“Tumeweka maafisa wa kupambana na moto kusaidia kuuzima,tulipata simu kuhusiana na moto huu mwendo wa saa moja na dakika thelathini na tano,” alisema Bw Nahid Musa, mkuu wa kitengo cha askari wa baraza katika kaunti ya Mombasa.

Bw Mussa alisema kuwa wazimamoto walikumbana na matatizo kidogo wakati wa kukabiliana na moto huo kutokana na upepo mkubwa uliokuwa unatoka baharini.

Maafisa wa polisi kutoka eneo la Kisauni pia walikuwa wamefika katika eneo la moto huo.

Wageni katika hoteli zingine zilizo karibu waliendelea na shughuli zao bila matatizo yeyote.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.