Wala pesa za Jubilee na kugeuka kumsifia Raila

Taifa Leo - - HABARI ZA KAUNTI - Na PETER MBURU

JUHUDI za mfanyabiashara mashuhuri kuwatongoza wapigakura wa makabila tofauti kando na jamii za Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake kaunti ya Nakuru, ziliambulia patupu baada ya mamia ya watu waliohudhuria kuondoka wakiimba nyimbo za kumsifu kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Ili kujionyesha kujitolea kusaidia kumtafutia kura rais Kenyatta, mfanyabiashara James Karimi aliwaalika mamia ya kina mama na vijana wa kutoka makabila tofauti kwenye hoteli ya Kunste iliyoko mjini Nakuru na kutenga jamii za Wakikuyu na Wakalenjin ambao tayari wanamuunga mkono rais.

Bw Karimi aliwanunulia vinywaji kisha kuwapa na kuwaweka mkutanoni kwa zaidi ya saa mbili, huku akitumia mbinu anuwai kuwafurahisha ili wabadili misimamo na kuamua kumchagua Rais Kenyatta.

Baadaye mfanyabiashara huyo anadaiwa kuwapa watu hao waliokuwa takriban 300 Sh300 kila mmoja kama njia ya kuwavutia kwenye chambo cha Jubilee na kubadili mawazo ili wamchague rais Kenyatta kwenye Uchaguzi ulioratibiwa kufanywa Oktoba 17.

“Kwa sasa hatuna haja na Wakikuyu, tunakimbizana na kura za makabila ambayo hayakumpa rais Kenyatta kura. Kumtafutia Kenyatta kura kwa Wakikuyu wakati huu ni kupoteza muda,” Bw Karimi akasema.

Kwa tamaa ya pesa na ili kumfurahisha na kumwonyesha kuwa wangefanya matakwa yake, wananchi hao walishangilia kila wakati wakisema kura zao watampa Rais Kenyatta.

Hata hivyo, wakitoka nje baada ya kukabidhiwa pesa, vijana na kina mama hao waliondoka wakiimba nyimbo za kumsifu kinara wa upinzani wakisema kura zao hazingenunuliwa kwa Sh300.

Taifa Jumapili ilishuhudia baadhi ya vikundi vya waliohudhuria vikizozana kuhusu ugawaji wa pesa hizo kwani waligawanywa kwa vikundi.

Duru za kuaminika ziliarifu kuwa mkutano huo ulikuwa njia ya ‘mahusiano ya umma’ (public relations) ili Bw Karimi ajijengee jina kwa rais kuwa alikuwa akimfanyia kazi miongoni mwa wananchi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.