Je, Muhoho anaandaliwa na jamii yake kuongoza 2O32?

Wachanganuzi wa kisiasa wanadai kuwa mrithi wa rais Uhuru, na msemaji wa jamii ya Mlima Kenya atakuwa mwanawe

Taifa Leo - - MAKALA MAALUM - Na MWANGI MUIRURI

HUKU Rais Uhuru Kenyatta akikaribia kustaafu kutoka kwa siasa, eneo la Mlima Kenya linaonekana dhahiri kuwa halitaponyoka siasa za ukiritimba wa aila fulani huku mrithi na msemaji wa kijamii akionekana kujitokeza kama mwanawe, Jaba Muhoho.

Kwa sasa, taswira inayojitokeza ni kuwa, kama hapatazuka msukumo mwingine wa kisiasa ambao utakaidi siasa hizo za kufuata ‘familia kubwa’, kuna uwezekano mkubwa kuwa eneo hilo litabakia kuwa chini ya udhibiti wa familia ya babake rais, Mzee Jomo Kenyatta.

Wadadisi wa kisiasa wanaonya kuwa ikiwa eneo hilo litajikomboa kutoka uthibiti wa siasa hizo, basi halina budi kujiweka tayari kukumbatia upana wa kimawazo na ambapo litashinikiza kuwe na uwazi katika urithi huo.

Mdadisi wa masuala ya kisiasa, Gasper Odhiambo anasema kuwa “ufunguo wa Mlima Kenya katika kujipa uhuru wa kisiasa uko mikononi mwa wenyeji hasa wale wa kawaida. Ni wao waamue kuendeleza siasa hizo za kuthibitiwa na familia kubwa, au wajikomboe wenyewe.”

Anasema kuwa hadi sasa kile ambacho kinajitokeza waziwazi ni kuwa “eneo hilo limepangiwa njama pana na ambayo inaonekana ikiwa na upana mkuu wa kufaulu ambapo Rais Kenyatta ameteka nyara eneo hilo kiuthibiti hadi mwaka wa 2032.”

Anaonya kuwa hilo lina maana kuwa baada yake kustaafu aidha baada ya uchaguzi mkuu wa kurejelewa Oktoba 17, 2017 iwapo atashindwa na upinzani, au mwaka wa 2022 iwapo ataibuka mshindi, bado uthibiti wake wa eneo hilo utabakia imara hadi kijana wake ajitose kwa uwanja.”

Anasema kuwa kuwa, lengo kuu la Rais Uhuru Kenyatta kung’ang’ania kufa kupona kumkabidhi naibu Ruto urithi ni kutekeleza njama ya kumweka pazuri Muhoho nafasi ya kuwa Rais wa hivi karibuni. Anawatahadharisha watu wa Mlima Kenya kuwa hadi sasa wameshuhudia njama kali za kuwaangusha vigogo ambao wamekuwa nao kisiasa na ambao walikuwa wamejijengea ushawishi wa kuibuka wasemaji rasmi wa jamii hizo.

Majina ambayo yako hatarini kufifia kisiasa eneo hilo na ambapo aliyekuwa Gavana wa Kiambu, William Kabogo anadai kuwa yaliangushwa kimakusudi kwa nia ya kuvuruga urithi wa usemaji wa jamii hizo ni pamoja na Peter Kenneth, Martha Karua, Kabogo mwenyewe na aliyekuwa mbunge wa Kigumo, Jamleck Kamau.

Kabogo anadai kuwa “kulizuka mtandao mkali wa njama na hila na ambao ukilenga kukwamiza walioonekana kuwa na ushawishi wa kijamii waliangushwa katika mchujo wa Jubilee Party na waliong’ang’ania kuwania kama wagombezi huru wakasukumwa kwa kampeni kali hadi nje ya mchezo.”

Anasema kuwa mpango pana ulikuwa wa kuweka “watu fulani katika mtandao wa urithi na wajithibiti kwa minajili ya kuibuka na mrengo wao wa baada ya rais Kenyatta pia wa siku za baadaye.”

Ingawa hajitumi kuwa mwazi kukariri kinaga ubaga kuhusu njama hiyo, anasema kuwa “huu wote ulikuwa ni mchezo wa 2022 na baadaye.”

Anasema kuwa kuanzia sasa, kuna miaka 15 ambayo imebakia hadi rais Kenyatta na William Ruto wamalizane na utawala na ambapo jamii za Mlima Kenya zisipochukua tahadhari, zitajipata zimekabidhi ushawishi wao kisiasa nje ya uthibiti wa kiserikali.

“Nimekuwa nikisema kuwa kama nyumba tunafaa kujijenga na tuwekeze rasilimali zetu za kisiasa katika msemaji thabiti ambaye atakuwa katika meza ya kuandaa mkataba wa urithi huo. Lakini nimechukuliwa kama mchochezi na ambaye anafaa kukemewa. Lakini taswira inayojitokeza ni kuwa, tusipojipanga, tutapangwa,” anasema.

Anasema kuwa hakuna geni ambalo yeye husema kila wakati, wala sio kwa nia mbaya kuteta kwamba “kama wanahisa katika urithi huo tunafaa kuwa na msemaji thabiti wa kijamii na ambaye ana tajriba na upana wa kimawazo wa kuelewa kuwa ni lazima kuwe na mkataba wa kimaelewano katika urithi huo.”

Hapo ndipo Odhiambo anasema kuwa “Kabogo anaogopa kuwa msema kweli wa dhati na ajieleze kwa ufasaha zaidi ili atoe ujumbe kuwa baada ya Ruto, anayeandaliwa ni mwanaye Rais, na ambaye ni Muhoho.”

Anasema kuwa iwapo njama hiyo ya Uhuruto haitapanguliwa, na ipate ufanisi wa utekelezaji, basi kuanzia mwaka wa 2032, eneo la Mlima Kenya litarejea ndani ya boma ya familia ya Kenyatta kusaka msemaji wa kijamii na pia mrithi wa urais.”

Anasema kuwa wale wote katika Mlima Kenya ambao kwa sasa wanamezea mate kiti hicho cha ikulu watakuwa wamezeeka kiasi cha kupoteza fahamu zao kisiasa.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa wawaniaji wa Jubilee 2017 eneo la Mlima Kenya, Samuel Maina, njama hiyo inayotekelezwa kupitia hila ya urithi ni njia tu ya kuendeleza utawala wa familia kubwa.

Asema: “Kwa sasa nafasi ya msemaji huyo wa kumrithi Uhuru ni finyu sana katika kuwania urais mwaka wa 2032 ambapo Rais anatazamia Jubilee kung’atuka kupitia miaka 10 ya naibu wake.

Walio pembeni kwetu ni kina Kenneth, Karua na wengine kama Paul Muite na labda na labda Amos Kimunya wa Kipipiri.”

Anasema kuwa miaka yao wote kwa sasa haiwapi nafasi ya kuwahi kuwa marais hapa nchini katika uchaguzi wa 2032 kwa kuwa watakuwa na kati ya miaka 75 na 90.

“Hii ina maana kuwa mrithi wa Rais katika usemaji wa Agikuyu ni lazima awe wa chini ya miaka 40 kwa sasa na ukiangalia mkusanyiko wa wanasiasa wa sasa katika eneo hili letu, wote ni wakongwe ambao hawana nafasi 2032. Hapo ndipo tumetegwa na ndoano ya Jaba Muhoho ambaye kwa sasa ako na miaka 21. Mwaka wa 2032 atakuwa na miaka 38 akiwa mwingi wa ujana wa kuvutia wapiga kura vijana na tajriba ya uongozi kupitia kusajiliwa na familia yao,” asema.

Kiongozi wa Vijana wa Jubilee 2017 katika eneo hilo, Dishon Warui anasema kuwa “sio siri kuwa Muhoho anaandaliwa kutwaa uongozi wa jamii za Mlima Kenya.”

Anasema kuwa hilo lilibainika mapema 2014 ambapo Rais Uhuru alikuwa na mazoea ya kuandamana na mwanaye huyo katika hafla muhimu za kiserikali na kisiasa.”

Asema: “Alikoma tu mtindo huo baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuanza kuangazia uwezekano wa njama hiyo kuwepo. Lakini hata kwa sasa tunajua kijana huyo huwa anatumwa katika hafla nyingi za majadiliano ya kisiasa na ambapo huwakilisha babake ambaye ndiye rais. Pasipo shaka yumo njiani anakuja jinsi Mzee Kenyatta alivyomtosa Uhuru katika

Picha/ Maktaba

Muhoho akimsalimia mkewe Rais wa Uganda Janet Museveni katika Ikulu ya Kampala wakati ziara ya Rais Kenyatta nchini Uganda Ikulu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.