Masaibu ya wagonjwa hospitalini, hata wanafunzi

Taifa Leo - - MAKALA MAALUM - Na NYABOGA KIAGE

MWANAFUNZI wa darasa la nane katika shule moja kule Kisii, ni miongoni mwa wanawake wanane ambao wamefungiwa katika wodi moja kwenye hospitali ya Christa Marriane.

Akiwa na mtoto wake aliyezaliwa wiki iliyopita, msichana huyo anahofia kuwa anaweza kukosa kuufanya mtihani wake wa darasa la nane mwezi ujao.

Akizungumza na Taifa Jumapili, mwanafunzi huyo anaeleza kuwa alihadaiwa kuwa alikuwa ameruhusiwa kwenda nyumbani lakini akaletwa kwenye chumba hicho ambacho sasa ni ‘nyumbani kwake’.

“Mama yangu alikuwa amekazana kuwaomba madaktari wanikubalie kuenda nyumbani huku nikizidi kusaka hela niwalipe. Waliponiambia kuwa walikuwa wananikubalia kwenda nyumbani sikuficha furaha yangu,” alisema mwanafunzi huyo.

Anaelezea jinsi wao huteseka huku wakilala kwenye magodoro matatu yaliyowekwa sakafuni.

Kulingana naye, wao huwa hawapati usingizi wa kutosha kwani watoto wao hulia kila usiku.

“Pia hatukubaliwi kutoka nje ya chumba hiki na hata mtu huomba ruhusa kwenda chooni tufanyavyo tukiwa shuleni,” alisema.

Bi Beatrice Sabato ambaye ni msimamizi mkuu katika hospitali hiyo, alisema kuwa walilazimika kuwapeleka wagonjwa hao katika chumba hicho kwa sababu wodi za hospitali hiyo zimejaa.

“Tuliwapeleka huko kwa sababu vitanda vyote vimejaa na tuko na mpango wakuwaacha waende nyumbani,” alisema.

Hospitali hiyo ya Christa Marianne, imekuwa ikiwasaidia wakazi wa eneo hilo, hasa baada ya wauguzi kwenye hospitali za umma kugoma.

Wagonjwa hutoka hata kaunti jirani za Narok, Nyamira na Migori kusaka matibabu katika hospitali hiyo.

Tulipozuru hospitali hiyo, tulishuhudia wagonjwa wakilala wawili wawili kwa kila kitanda.

Bw Kelvin Ochieng, ambaye mke wake alijifungua hivi majuzi alisema kuwa inamlazimu mtu kumfuata daktari na kumuomba amuone mgonjwa wake kwa sababu ya idadi kubwa ya wagonjwa katika hospitali hiyo.

“Ni kweli kuwa wagonjwa ni wengi na usipomfuata daktari huku ukimuomba amshugulikie mgonjwa wako atakaa sana bila kuonekana,” alisema Bw Ochieng.

Haya yaliungwa mkono na akina mama wengine ambao wamefungiwa katika hospitali hiyo huku wakisema kuwa bado walikuwa na maumivu mengi.

Msichana wa miaka 16 ambaye pia amekaa humo kwa wiki mbili sasa, anasema wagonjwa hulazimika kula chakula kwa pamoja kwa kukosekana chakula cha kila siku.

Mmoja wetu akitembelewa tunakula sote, huku tukitarajia kuwa jamaa zetu watapata pesa iliwatuondoe huku,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.