Mungu aachiwe nafasi ayatawale maisha yetu yote, tumaini liwe kwake

Asiwe Mungu wa Jumapili au Ijumaa tu bali wa kila siku

Taifa Leo - - DINI - Padre Faustin Kamugisha

Mtoto mdogo ambaye baba yake alikuwa mbali na nyumbani kila mara, alitazama picha ya baba yake kwenye fremu ya picha ukutani na kumwambia mama yake, “Mama, natamani baba angetoka kwenye fremu ya picha hiyo.”

Je, Mungu ni wa kweli kwako, nafsi ambayo iko karibu nawe, au Mungu ni kama picha kwenye fremu ya picha ukutani, kauli mbiu, fundisho au jambo la kutazama na kustaajabia lakini bado liko kwenye fremu tu.

Je, umewahi kutamani kuwa Mungu angetoka kwenye fremu na kuwa ukweli unaoishi kwa utukufu? Je, umelia, “Ee ningejua mahali pa kumpata?”

Mungu asiwe Mungu wa Jumapili tu. Mungu asiwe Mungu wa Ijumaa tu. Mungu asiwe Mungu wa kusoma kwenye Biblia takatifu tu. Mungu asibaki kwenye wimbo wa taifa tu. Mungu asibaki kwenye kadi za kutakiana amani tu. Mungu asibaki kwenye filamu tu. Mungu asibaki kwenye ujumbe wa simu tu. Mungu asibaki kwenye makala ya kidini. Mungu asibaki tu kwenye hotuba za kuomba baraka. Mungu asikimbiliwe kama parachuti wakati ndege ipo katika hatari ya kudondoka. Mungu asitumiwe kama boya.

Mungu atawale maisha yetu ya kila siku. Mungu atawale kwenye siasa. Mungu atawale kwenye biashara. Mungu atawale kwenye kilimo. Mungu atawale kwenye michezo. Mungu alipoumba samaki alizungumza na bahari. Mungu alipoumba miti alizungumza na udongo. Mungu alipomuumba mtu alizungumza na nafsi zake.

“Na tuumbe mtu kwa mfano wetu,” (Mwanzo 1:26).

Ukimtoa samaki toka kwenye maji atakufa. Ukiutoa mti kutoka kwenye udongo utakufa. Ukimtoa mtu kwa Mungu unammaliza. Ni katika Mungu kuliko na uzima. Mungu bila binadamu bado ni Mungu. Lakini binadamu bila Mungu si chochote.

Kuna methali ya Kiswahili isemayo: “Mungu hajesha kuniumba.” Mungu hajamaliza kuniumba. Kila mara Mungu huendelea kutubadilisha tuwe bora zaidi.

Methali hii hutumiwa pale mtu anapokuwa na matumaini ya kupata baraka kutoka kwa Mwenyenzi Mungu. Ni himizo kuwa Mungu hajamaliza kutubariki na daima yuatuwazia mema.

Hujafa hujaumbika; Mja haishi kuumbwa. Ni katika msingi huu mtume Paulo alisema: “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu,” (1 Wafilipi 1:6).

Sharon Farley alisema, “Nilipokuwa nazungumza na Mungu asubuhi moja, nilifikiria kile ninachohitaji kutoka kwa watu. Hiki ndicho nilichokiandika: Watu watambue uwepo wangu, wanikiri, wajue ambalo nimelifanya, wajue ambalo naweza kufanya. Kwa wewe Mungu kujua ninavyohisi. Kunipa muda wako, kunisaidia, kunikubali, kujua kuwa ninakujali, kutotilia maanani lile ambalo hulielewi kuhusu mimi na kuniamini.

Na Mungu aliniambia: ‘Sharon, tazama ulichokiandika, kisome mara mbili. Hiki ndicho nahitaji kutoka kwako.” Kwa ufupi sisi tutambue uwepo wa Mungu, tumkiri, tumpe muda wetu, tumkubali.

Kuna aliyesimulia alichokiona kwenye mashindano ya mpira wa miguu. “Nilikuwa naangalia mpira wa miguu katika uwanja wa shule. Nilipokaa, nilimuuliza kijana mmoja juu ya matokeo ya mchezo. Kwa tabasamu, alijibu ‘Wako mbele yetu 3-0!’

Nikasema: ‘Kweli! Mbona huonekani kukata tamaa?’ ‘Kukata tamaa?’ Yule mvulana aliuliza kwa mshangao. ‘Kwa nini nikate tamaa wakati bado refa hajapuliza kipenga cha mwisho? Nina imani na timu yangu na meneja wa timu; nina hakika tutashinda.’ Na kweli mchezo uliisha kwa mabao 5-4 timu ya kijana ikiwa mbele! Alinipungia mkono taratibu, na tabasamu nzuri akiondoka uwanjani; nilishangaa, ujasiri mkuu kiasi hiki.

“Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu...” (1 Wafilipi 1:6)

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.