‘Baba’ waache machangudoa wa kisiasa warejee walikotoka

Taifa Leo - - KINAYA - Douglas Mutua

BABA’ usitie shaka, upepo utapita tu. Hao wanaokutoroka usiwajali, waache waende waendako. Kisa na maana? Kuna kuhama na kuhamishwa.

Kwamba wamehamia kwako wakakaa siku mbili kisha wakarejea walikotoka ni ishara kuwa hawangekufaa kitu.

Tena, hawajauhama muungano wako wa Nasa kwa hiari, wamehamishwa na shida zao. Ni kina pangu pakavu tia mchuzi ambao - kama changudoa wanaofanya biashara isiyohitaji mtaji pale mtaani Koinange jijini Nairobi -hupelekwa huku na huko na matumbo yao.

Hao, ndio wakora haswa wasiojua chochote kuhusu umuhimu wa kutozisaliti nafsi zao. Hawali wakashiba, hata mashuzi yakiwajia juu kisha wakutane na vyororo watafundira tu! Ni vyema kwamba wameondoka kabla ya kuwaambukiza wafuasi wako maradhi ya kuhamahama.

Mwanamume anapotokea mbele ya kamera za runinga na kutangazia umma eti chama cha kisiasa kilimpokonya mke, anapaswa kutueleza iwapo alikohamia ameahidiwa mke.

Vilevile, anapaswa kutwambia peupe kipweza chake kilitwaliwaje na wanasiasa wenzake ikiwa yeye ni dume kamili. Kazi si kututumua misuli tu! Ya unyumba usipoyaweza, labda kwa kuishiwa na maarifa na donge, usithubutu kuwalaumu wengine.

NASA ingekuwa na haja ya kuiba wake wa watu ingewaoza wakuu wake waliopokezwa kichapo cha mbwa aliyeingia msikitini wakakimbilia polisi! Unawajua.

Visa kama cha Weta kushtakia kwa walinda usalama vingekuwa nadra au havingetokea kamwe. Lakini najua ni njaa tu, yaani siasa za tumbo.

Ukitaka msaada wa kifedha, chukua bakuli kubwa ukalie miguu kwenye kona ya mtaa wowote wenye idadi kubwa ya watu jijini Nairobi, hutakosa wa kukurushia angaa Sh20.

Utakachohitajika kufanya ni kuvumilia jua. Hata ‘Baba’ mwenyewe alipopungukiwa na pesa za kampeni alilazimika kuvumilia dhihaka za mibabe wa Jubilee waliomwita ombaomba.

Lakini hilo halikumvunja moyo; wafuasi wake walisema ‘kula tano, ‘Baba’ tano’.

Kila mtu anajua kwamba Ndolo, aliyekuwa mbunge wa Makadara, hana hata kura zao za kumpa ‘Ithe wa Jaba’.

Kwamba amekosana na ‘Baba’ – labda kwa kukosa sadaka ya kuchangia kopo la mwana huyo wa Jaramogi – si lazima avuke upande wa pili huku akieneza uvumi hata wa kwake nyuma ya pazia.

Ni sawa na mke kutalikiwa na kuanza ‘kumvua nguo’ aliyekuwa mumewe, akidhani kwa kufanya hivyo atapendwa na mume wa sasa. Wajuao mambo ya ndoa watakwambia hatutaki upuuzi huo; utafyata domo nile kitumbua kwa amani au ukirejeshe ulikokitoa, ni vingi haviishi!

Ikiwa uliamini kwamba ‘Ruto Mzuri’ angesubiri hadi ‘Baba’ aunde serikali na kumpa cheo, jiulize iwapo unatumia akili kama kofia. Nilijua ni mjanja tangu mwanzo.

Angekuwa na nia njema, hangewania ugavana wa Bomet Agosti 8. Angesubiri wafike Kanaani na ‘Baba’ alishwe manna, maziwa na asali. Yamkini vitamutamu vyote hivyo vimechelewa, simba akaamua kula nyasi.

Usimshangae Munya kwa kurejea alikotoka, wiki moja tu baada ya kuondoka Jubilee kwa vishindo vya mashua na kuingia kwa ‘Baba’ akizungumza lugha ya mabadiliko. Busara za Wakamba huniambia nyani ni nyani tu angavishwa rinda jema. Mwache amumunywe!

Mwangalie Hassan Sarai Omar, mtoto wa chekechea aliyetaka kuingia chuo kikuu moja kwa moja. Siasa za Afrika ni sharti upande ngazi hatua kwa hatua.

‘Baba’ anapaswa kuwaambaa kama majini wote wanaokimbia kwake wakisema Jubilee iliiba kura zao; Jubilee ikiwapa ‘pole’ mifukoni watairudia upesi.

mutua_muema@yahoo.com

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.