Alima soja mangumi kuzuia demu langoni

Taifa Leo - - DONDOO! - NA LEAH MAKENA

KIOJA kilishuhudiwa kwenye ofisi moja eneo hili, polo na soja waliporushiana mangumi bawabu alipomzuia jamaa kuingia na mpenzi wake ofisini.

Duru zasema kuwa bosi wa polo alikuwa ziarani kwa muda wa wiki mbili na hivyo polo akaamua kwenda na kidosho ofisini ili aweze kumtambulisha kwa wafanyikazi wenzake.

Asubuhi ya kioja, jamaa huyo alifika akiwa amemkumbatia mrembo wake huku wakitembea kwa madaha na kumtaka soja kuwapisha bila hata kumwamkua.

Inasemekana kuwa, polo alijawa na mori kutokana na dharau aliyoonyeshwa na wapenzi hao na kubana mlango ghafla baada ya polo kupita. Inasemekana kuwa jamaa alitaka kujua sababu ya kero hilo na bila kusita akapata jawabu kutoka kwa soja.

“Hapa ni kazini na wala si sehemu ya burudani. Kama ulitaka kutuonyesha mrembo wako, mbona hukufanya hivyo wakati bosi alikuwa hapa? Mwambie atoe kitambulisho cha kazi na nitamruhusu kupita,” soja alisema.

Hapo ndipo polo alianza kumrushia mangumi na soja akamchangamkia, vita vilivyofanya waliokuwa karibu kuacha kazi zao kuwatenganisha. Licha ya polo kulalamikia aibu aliyokuwa amepata, soja alisisitiza kuwa kamwe hangekubali mtu asiyemfahamu kuingia ofisini.

Baada ya vuta nikuvute kwa muda, soja aliamua kumvutia bosi waya na kusimulia sinema iliyokuwa imeshuhudiwa. Duru zasema kuwa polo alipata simu mara moja kutoka kwa bosi akitakiwa kwenda nyumbani na kungoja kesi yake kuamuliwa baada ya wiki mbili.

Walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa jamaa alilazimika kurejea nyumbani akiwa na mrembo wake huku akitishia kumtia soja adabu iwapo angepigwa kalamu.

Kidosho alisalia kimya kwa muda wote huo huku akijutia hatua yake ya kuandamana na mpenzi kazini kwake.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.