IEBC kwenye mtanziko huku kura za marudio zikikaribia kwa kasi kuu

Wadadisi wa kisiasa wanasema tume hiyo inapaswa kuisafisha nyumba yake kwanza kabla ya marudio ya uchaguzi

Taifa Leo - - JAMVI - Na BENSON MATHEKA

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), haina budi kudumisha maadili ya hali ya juu katika marudio ya kura ya urais ili kuepuka fedheha kama iliyopata baada ya matokeo ya kura kubatilishwa na Mahakama ya Juu, wadadisi wanasema.

Wachanganuzi wa kisiasa wanasema tume hiyo inapaswa ‘kusafisha nyumba yake’ kwanza na kuhusisha wadau wote huku ikidumisha uhuru wake kwa kutoonekana kuegemea upande wowote.

“IEBC haifai kupuuza shinikizo kutoka kwa upinzani na mashirika ya kijamii. Hawa wote ni wadau katika uchaguzi. Kwa kuwapuuza, inaonyesha inaegemea upande wa Jubilee. Inapaswa kuwa tume huru na uhuru huo unafaa kuonekana katika utendakazi wake,” anasema Bw Shadrack Simba, mdadisi wa masuala ya siasa.

Anasema tume haifai kupuuza tishio la muungano wa NASA la kususia uchaguzi ulioratibiwa kufanyika Oktoba 17 ikiwa matakwa yao hayatazingatiwa.

“Shinikizo kutoka kwa NASA ni kwa sababu katika maandalizi ya uchaguzi wa Agosti 8, IEBC iliwapuuza. Aidha, mahakama ilisema kulikuwa na dosari katika uchaguzi huo na kwa hivyo, njia ya kuepuka hali kama hiyo ni kusikiliza pande zote mbili,” asema Bw Simba.

NASA imesema haitashiriki marudio ya kura ya urais ikiwa maafisa waliovuruga uchaguzi hawataondolewa. Inataka Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Ezra Chiloba, naibu wake Betty Nyabuto, Mkurugenzi wa teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT) James Muhati, mkurugenzi wa masuala ya kisheria Praxedes Tororey na mwenzake wa uchaguzi Immaculate Kassait miongoni mwa wengine, wafutwe kazi .

Kiongozi wa mawakili wa NASA, Bw Paul Mwangi, alisema wana ushahidi wa kuwashtaki maafisa hao kwa kuvuruga uchaguzi ambao matokeo yake yalibatilishwa na Mahakama ya Juu Septemba 1.

Hata hivyo, japo awali mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alionekana kuchukua hatua kwa kuteua kamati ya kusimamia uchaguzi alionekana kusalimu amri kutoka kwa viongozi wa Jubilee waliosisitiza kuwa tume haifai kufanyiwa mabadiliko.

“Bw Chebukati alianza vizuri baada ya uamuzi wa Mahakama ya Juu kwa kutangaza kwamba wote waliotenda makosa yaliyofanya matokeo kubatilishwa watachukuliwa hatua. Hata alimwandikia barua Bw Chiloba akitaka ajibu masuala kadhaa. Hata hivyo, mambo yalibadilika mgawanyiko ulipozuka kati ya makamishna baadhi wakimtetea Bw Chiloba,” asema Bw Geff Kamwanah, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

Anasema japo IEBC inasema inasubiri uamuzi wa kina wa Mahakama ya Juu kabla ya kuchukua hatua, dalili ni kwamba haiko tayari kuwaadhibu waliohusika akiwemo Bw Chiloba ambaye amelaumiwa pakubwa. Lakini Bw Mwangi anasema wana mengi dhidi ya Bw Chiloba ikiwa ni pamoja na kukaidi agizo la Mahakama wakati wa kesi.

“Tutamshtaki Chiloba na Muhati kwa kudharau mahakama kwa sababu walikataa kutii agizo la Mahakama ya Juu lililowataka wafungue mitambo ya IEBC ili ikaguliwe,” akasema Bw Mwangi, ambaye ni miongoni mwa mawakili waliowakilisha mgombeaji urais wa NASA , Raila Odinga, katika kesi iliyofanya ushindi wa Rais Kenyatta kubatilishwa.

“Tunataka wafungwe jela kwa sababu kuna ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha walikaidi mahakama,” akasema Bw Mwangi.

Aliongeza kuwa wanaendelea kukusanya majina ya maafisa 1,000 waliosimamia uchaguzi katika vituo vya kupigia na kujumlisha matokeo ambao walikataa kupeperusha matokeo halali ya kura ya urais hadi kituo cha kitaifa.

Wakiongea baada ya kuongoza mkutano wa kundi la wabunge wa muungano huo jijini Nairobi Jumatano, viongozi wa NASA walisema hawatakubali kushiriki uchaguzi maafisa hao wakiwa ofisini.

“Tumesoma sehemu ya uamuzi wa Mahakama ya Juu na tumetambua watu ambao waliohusika na wizi wa kura katika IEBC. Tumeagiza mawakili wetu kuanza utaratibu wa kuwashtaki watu hao kwa sababu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) amekataa kufanya hivyo,” alisema kinara mwenza wa muungano huo, Moses Wetang’ula.

NASA imekuwa ikimtaka Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Bw Keriako Tobiko kuwashtaki maafisa wa IEBC waliovuruga matokeo ya kura ya urais ilivyoagiza Mahakama ya Juu.

“NASA inataka Wakenya wajue hakutakuwa na uchaguzi iwapo matakwa yote tuliyozua katika kesi yetu hayatatimizwa,” alisema Bw Wetang’ula.

Bw Kamwanah asema japo baadhi ya matakwa ya NASA huenda yakaingilia uhuru wa tume na mengine yasiweze kutimizwa kwa sababu ya muda, IEBC haina budi kushirikisha muungano huo katika maandalizi na kwa uaminifu wa dhati.

“Kwa mfano, kuajiri maafisa wapya 290 wa kusimamia vituo kujumlisha matokeo huenda ikiwa ni mlima kwa tume katika maeneobunge yote 290. Sio wote waliovuruga matokeo na hili ni suala linaloweza kutatuliwa IEBC ikiwa na uwazi katika shughuli zake,” asema.

Anasema kujiunga kwa mashirika ya kijamii kushinikiza mabadiliko katika IEBC na tisho la upinzani kususia marudio ya kura kunapasa kuzindua tume ili iandae kura hiyo kwa uadilifu.

Mnamo Jumatano, kundi la Kura Yangu Sauti Yangu linaloshirikisha mashirika kadhaa ya kijamii lilifanya maandamano jijini Nairobi hadi ofisi za IEBC likitaka tume ifanye mabadiliko kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Juu.

Aidha, wanachama wa kundi hilo walifika katika ofisi za Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kushinikiza awashtaki wote waliovuruga uchaguzi wa Agosti 8 na kusababisha matokeo ya kura ya urais kubatilishwa na Mahakama ya Juu.

PICHA/DPPS

Naibu Rais William Ruto na viongozi wengine wa Jubilee alipokutana na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati (kulia) na makamishna wengine jijini Nairobi majuzi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.