Jubilee na Nasa sasa waamua sera kando propaganda mbele

Mirengo hiyo miwili haizungumzii tena manifesto kama vile elimu bali kueneza jumbe za kudhalilisha washindani

Taifa Leo - - JAMVI - Na LEONARD ONYANGO

HUKU kampeni kwa ajili marudio ya uchaguzi wa urais zikishika kasi, mirengo ya National Super Alliance (NASA) na chama cha Jubilee sasa imetupilia mbali manifesto zao na sasa wanatumia propaganda kupigana vikumbo.

Tofauti na kampeni za uchaguzi wa Agosti 8 ambao matokeo yake yalifutiliwa mbali, ambapo kambi za Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa NASA Raila Odinga zilishindana kwa manifesto sasa zimekumbatia propaganda katika mitandao ya kijamii na hata mikutano ya kisiasa.

Katika kampeni zake kabla ya uchaguzi wa Agosti 8, Rais Kenyatta aliahidi Wakenya kutoa elimu ya bure katika shule za upili, kuwasaidia wanafunzi wa vyuo vikuu kupata mafunzo ya nyanjani na kuwalipa mshahara kwa karibu miaka.

Rais Kenyatta pia aliendesha msururu wa matangazo ya kuwaeleza Wakenya mafanikio ya serikali yake tangu Jubilee kuchukua hatamu za uongozi mnamo 2013.

Naye Bw Odinga aliahidi kutoa elimu ya bure, chakula na sare kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, kuwasaidia wajane na akina mama wasioolewa.

Lakini, tangu Mahakama ya Juu kufutilia mbali matokeo ya urais ya uchaguzi wa Agosti 8, Rais Kenyatta na Bw Odinga sasa hawazungumzii manifesto yao na badala yake wanashindana kwa kutumia propaganda.

Katika kikao cha Jubilee uwanjani Uhuru Park, Nairobi, wikendi iliyopita, Naibu wa Rais William Ruto alidai kuwa Bw Odinga hakufanya mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE).

“Nataka kumwambia bwana kitendawili aache kuzungusha fitina akiwataka watoto wasifanye mtihani. Ninataka kusema katika uwanja huu wa Uhuru Park kuwa Bw Odinga hakufanya mtihani wa kitaifa wa kukamilisha masomo ya shule ya msingi na sekondari,” akasema Bw Ruto.

“Kama Bw Odinga alifanya mtihani awaonyeshe Wakenya vyeti vyake vya KCPE na KCSE,” akaongezea. Madai hayo ya Bw Ruto yalilazimu kambi ya NASA kusambaza picha inayoonyesha Bw Odinga akiwa na wahadhiri wenzake wa Kitivo cha Uhandisi kat ika Chuo Kikuu cha Nairobi mnamo 1972, ili kuthibitisha kwamba Bw Odinga alienda shuleni.

Wiki iliyopita, barua inayosadikiwa kuandikwa na upande wa Jubilee ilichipuka katika mitandao ya kijamii huku ikidai kuwa mmoja wa vinara wa NASA Musalia Mudavadi amegura muungano huo wa Upinzani.

Saa chache baadaye Bw Mudavadi alijitokeza na kukana barua hiyo iliyokuwa imetiwa saini bandia.

Wanablogu wa Jubilee pia wamekuwa wakisambaza nakala za majarida mitandaoni yanayodai kuwa Bw Odinga alikutana na Rais Kenyatta faraghani na kumsihi kuunda serikali ya mseto.

Upande wa NASA umekuwa ukisambaza barua mbalimbali kuandikwa mitandaoni zinazodaiwa na Jubilee.

Barua ya hivi karibuni ni ile inayodaiwa kuandikwa na Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju ikiwataka wanasiasa wa chama hicho kuunga mkono hatua ya Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu kutaka kumwondoa afisini Jaji Mkuu David Maraga.

“Mnafahamu kuwa Jubilee tumeanzisha mchakato wa kutaka kumtimua Jaji Mkuu David Maraga kupitia kwa mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu.

“Lengo la barua hii ni kuwahimiza kuwa wageni katika vituo vya redio vya lugha ya kiasili, kutetea ajenda hiyo ya chama cha Jubilee,’ akasema barua hiyo ambayo imepuuziliwa mbali na Jubilee.

Barua nyingine ambayo imekuwa ikisambazwa na kambi ya NASA ni ile inayohimiza wakuu wa polisi kutoa ulinzi machifu na manaibu wao wanaodaiwa kununua vitambulisho vya kitaifa katika ngome za Upinzani. Hata hivyo Jubilee, wamejitenga na barua hizo.

Kulingana na mtaalamu wa masuala ya kisiasa na Mhadhiri Edward Kisiang’ani, Jubilee na NASA wanalenga kujipatia kura kwa kuibua hisia miongoni mwa wapigakura na wala si kwa kutumia manifesto.

“Mathalani, Jubilee wanapozuru ngome zao wanadai kuwa Mahakama ya Juu iliwapokonya ushindi wao. Lengo kuu la maelezo hayo ni kuibua hisia na kuwafanya wafuasi wao kujitokeza kwa wingi Oktoba 17 kumpigia tena kura Rais Kenyatta,” anasema Prof Kisiang’ani.

Anasema kuwa upande wa NASA umekuwa ukijikita katika suala ya Jaji Mkuu Bw Maraga ili kujishindia kura za jamii ya Abagusii katika Kaunti za Kisii na Nyamira. Mmoja wa vinara wa Nasa, Bw Musalia Mudavadi (kati) pamoja na viongozi wengine wa kisiasa wahutubia wanahabari katika majengo ya Bomas of Kenya mnamo Agosti

11, 2017.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.