Maraga alivyohakikisha siri kuu inadumishwa wakati wa kuamua kesi

Taifa Leo - - JAMVI -

Alhamisi usiku katika kikao chao cha kutoa uamuzi wa mwisho, Jaji Mkuu alitoa mwelekeo kama Rais wa Mahakama ambao uliwashawishi majaji wawili pamoja na naibu wake.

Wandani wa mahakama hiyo wanasema pindi mawakili walipomaliza kutoa hoja zao, Bw Maraga na Jaji Mwilu walikuwa tayari wamekata kauli kuwa mchakato wa uchaguzi ni muhimu kuliko matokeo yake, na iwapo uchaguzi ulifeli basi matokeo yake si halali.

Uamuzi wa Jaji Wanjala kuunga upande wa Jaji Mkuu ulichangiwa sana na wasiwasi wake kuhusu msimamo aliochukua katika kesi ya kupinga uchaguzi wa urais mnamo 2013 ambao ulimtia motoni.

Jaji Mohammed Ibrahim hangeweza kuhusika katika uamuzi wa mwisho kwa sababu alikuwa mgonjwa, hivyo, aliyelengwa na Jubilee ni Jaji Lenaola ili kuungana na majaji Ojwang’ na Bi Ndung’u kupinga Maraga na kundi lake.

“Jaji Lenaola ndiye aliyekuwa kigezo kikuu kuhusu mwelekeo wa mwisho wa korti,” akasema Apollo Mboya, aliyekuwa mwenyekiti wa Muungano wa Mawakili nchini.

“Iwapo angekubali ashawishike, pangekuwa na uumuzi wa sare miongoni mwa majaji na hiyo ingemaanisha matokeo ya uchaguzi yasalie yalivyo,” akaongeza Bw Mboya.

Jaji ‘msaliti’ anadaiwa kuwadokezea baadhi ya mawakili wa Jubilee na IEBC kuhusu hatima ambayo ilimkera sana Rais Kenyatta aliyekuwa akifuatilia matokeo hayo katika nyumba ya dadake.

Jaribio la mwisho kuwashawishi baadhi ya majaji liligonga mwamba na wanasiasa wa Jubilee wakiwemo Aden Duale na Kipchumba Murkomen pamoja na mawakili kadhaa waliamua kususia kikao cha Mahakama ya Juu mnamo Ijumaa baaada ya kudokezewa uamuzi uliokuwa umechukuliwa.

Muungano wa NASA vilevile ulidokezewa mapema kuhusu ushindi wake na mmoja wa mawakili wake, hatua iliyopelekea vinara wa upinzani kufurika kortini hata wakashindwa kuzuia furaha yao nyusoni.

Ijumaa asubuhi Jaji Mkuu alimpigia simu Jaji Mohamed kumfahamisha uamuzi wa korti na kumtakia nafuu ya haraka.

Saa tano na dakika 21, majaji wa Mahakama Kuu waliwasili kortini kutoa uamuzi wao huku Wakenya wakifuatilia kwa hamu katika runinga zao kote nchini.

Kulikuwa na wasiwasi mkubwa kortini huku mawakili wa IEBC na wale wa Rais Kenyatta wakionekana kushindwa kujitambulisha.

Seneta wa Siaya James Orengo ambaye aliongoza kikosi cha upinzani kortini, alitambulisha wenzake kortini kwa furaha huku akiwataja kila mmoja kwa jina.

Lakini wakili mkuu wa IEBC Paul Muite alionekana mwenye kiwewe huku akishindwa kuwatambulisha wenzake kwa korti kama ilivyo mtindo, kwa kusingizio cha ‘kuokoa wakati’

Hata hivyo aliagizwa na Jaji Mkuu kusoma orodha kamili ya wenzake.

“Ukuu wa nchi unategemea utiifu wa katiba yake na umakinifu mkubwa wa kufuata sheria, na zaidi ya yote, kumuogopa Mungu,” ni kauli ya Bw Maraga iliyotikisa mahakama kabla ya kutoa uamuzi uliorejesha Wakenya kwenye debe kumchagua rais tena.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.