Ajabu ya wajuao kukashifu ila hawana uwezo kutenda

Taifa Leo - - WATOTO - Na NYARIKI ENOCK NYARIKI

KUFIKIA saa tisa ushei, uga wa Mavuno ulikuwa umefurika watu ikakosekana nafasi ya kugeuza shingo wala ya kutema mate.

Kutoka kwenye vilima vya Mavuno, vichwa vya mashabiki vilionekana kama vichwa vya chungu waliohemera kwa kuyabeba machicha ya nazi. Majilio ya Mheshimiwa Gume Mbuguma, Gavana wa Mavuno, yalifuatwa na vifijo, mbwembwe, nderemo, jazba, mihemko, hoihoi na shangwe. Jumla ya maandalizi yaliyofanywa kutwa hiyo yalikamilika.

Mheshimiwa Gume Mbuguma alitembea mpaka katikati ya uwanja ambapo aliwasalimu wachezaji wa timu zote mbili ambao walionekana kuwa na nyuso zilizonyinyirika kama ngozi ya chatu. Kisha, alirudi chini ya jukwaa na kuketi kwenye kiti kilichokuwa kimetengwa kwa watu wenye mbeko kama yeye.

Saa kumi juu ya alama, refa alipuliza kipenga na mchuano ukaanza. Mashabiki wa timu zote mbili walizishangilia ili kuzitia hamasa.

Mnamo dakika ya kumi na tano, Joe Mikambe wa timu ya Gunge FC aliwapiga chenga wachezaji wa ngome ya Gwiji FC kisha akafyatua ‘kombora’ zito la kimo cha kuku na kumwacha mlinda lango wa timu ya Gwiji amelala yombo upande wa kulia. Mambo yakawa bao moja kwa nunge!

Timu ya Gwiji ilijitahidi kwa jino na ukucha kulikomboa bao lile ila mambo yalizidi kuiendea mrama. Safu yao ya mbele ilifanya makosa mengi yaliyoifanya kupoteza mabao mengi. Miongoni mwa mashabiki wa timu ya Gwiji, alikuwamo bwana mmoja aliyevalia kaputi lililomfunika hadi kwenye vifundo vya miguu. Bwana huyu alionekana kuchachawa kwa hasira. Kinywa chake hakikuisha kububujikwa na maneno ya kuwakashifu wachezaji wa timu ya Gwiji.

“Mwone yule bwege! Badala ya kutoa pasi upande wa kushoto ameishia kuupoteza mpira mzuri bure ghali.’’

Mashabiki wa timu ya Gwiji walivutiwa sana na kauli alizozitoa yule bwana aliyevalia kaputi. Walimwona kama mtu pekee ambaye angeweza kuikomboa timu yao ambayo ilikuwa inaendelea kutapatapa jinsi mfa maji anavyotapatapa kuushika unyasi ili asizame majini.

“Jamani ee! Huyu bwana anaweza kuwa winga hodari sana wa kushoto. Ninamwomba meneja wa timu akamjaribu,’’ shabiki mmoja alitoa maoni.

Ombi liliitikiwa. Bwana aliyevalia kaputi alikabidhiwa jazi la timu ya Gwiji na kuombwa kukikomboa kihori cha timu kilichovuja maji. Mwenye kaputi alisitasita na kuzubaa. Joto lilipoendelea kuelekezwa kwake, aliinama chini ya kiti alichokikalia na kuuchukua mkongojo wake na kujikongoja kwenda zake. Kumbe yule mchezaji wa mpira wa ‘mdomo’ alikuwa kiguru!

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.