Mbunge kufichua siri ili aondoe Urusi, mshukiwa katika lawama

Mwanasiasa huyo wa Republican analenga kushawishi serikali kutomchunguza Assange

Taifa Leo - - HABARI ZA AFRIKA NA DUNIA - Na AFP

MBUNGE mmoja nchini Amerika atatoa habari kuhusu madai ya udukuzi wa habari za siri za aliyekuwa mgombeaji wa urais Hillary Clinton wakati wa kampeni za urais, Jarida la Wall Street liliripoti Ijumaa.

Dana Rohrabacher, ambaye ni mbunge wa chama tawala cha Republican, Ijumaa alisema atatoa habari hizo za siri zilizofichuliwa na Wikileaks kusudi serikali ya Amerika isitishe uchunguzi dhidi ya kiongozi wa shirika hilo, Julian Assange.

Chini ya mpango huo Assange anapangiwa kutoa ushahidi utakaoondolea Urusi lawama kutokana na tuhuma kwamba ndiyo iliyosambaza jumbe za barua-pepe zilizochapishwa na shirika moja la kijasusi mwaka jana.

Kuchapishwa kwa jumbe hizo kuliathiri pakubwa kampeni za Bi Clinton aliyewania urais kwa tiketi ya chama cha Democrat.

Kulingana na ‘Wall Street’, Rohrabacher anataka “Rais wa Amerika Donald Trump amsamehe Assange kwa kusitisha uchunguzi dhidi yake”.

Wizara ya Haki ya Amerika imekubali kwamba inamchunguza Assange na kundi la Wikileakes kwa kufichua stakabadhi za siri za serikali ya Amerika kwa kudukua mitambo ya kielektroniki na barua-pepe ambazo Bi Clinton alikuwa akituma alipohudumu kama Waziri wa Mashauri ya Kigeni.

Kufikia sasa hakuna mashtaka yaliyopendekezwa dhidi ya Assange. Lakini inaaminika kuwa Amerika imeiomba Uingereza kumkamata raia huyo wa Australia endapo atatoka katika ubalozi wa Ecuador jijini London ambako amekuwa akiishi kwa miaka mitano.

Maafisa wa kijasusi wa Amerika wamehusisha Urusi na wizi wa jumbe za mawasiliano za Clinton na stakabadhi husika mwaka jana. Inaaminika kuwa taifa hili lilifanya hivyo kwa lengo la kuhujumu

nafasi ya Bi Clinton kushinda urais katika uchaguzi wa Novemba 8, mwaka jana.

Maafisa hao wanasema Wikileaks ilishirikiana na maafisa wa ujasusi wa Urusi katika kufanikisha uchapishaji wa habari hizo za siri. Wikileaks imekana habari hizo za siri zilizowasilishwa kwake na serikali ya Urusi. Hata hivyo, shirika hilo limesisitiza kuwa kamwe halitafichua chanzo cha habari ambazo huchapishwa katika mitandao yake.

Jarida hilo lilisema Rohrabacher alithibitisha kuwa aliongea na mkuu wa wafanyakazi katika Ikulu ya White House John Kelly wiki hii. Hata hivyo, hakufichua masuala ambayo walijadili.

Rohrabacher alimtembelea Assange mjini London mwezi jana.

“Rais wa Amerika Donald Trump amsamehe Assange kwa kukomesha kesi dhidi yake” Mbunge Dana Rohrabacher

Picha/maktaba

Mwasisi wa Wikileaks, Julian Assange akihudhuria kikao cha wanahabari ndani ya ubalozi wa Ecuador jijini London, Uingereza mnamo Agosti 18, 2014.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.