Hamu ya mume sina tena naye bado ananipenda

Taifa Leo - - FUMBO & FALAKI -

Shangazi mimi nimeolewa kwa miaka mitatu na nina mtoto mmoja. Tatizo ni kuwa sina hisia kabisa kwa mume wangu ingawa yeye ananipenda sana. Damu yangu imemkataa kabisa. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hiyo ni hali yenye utata sana hasa kwa sababu hamjakosana, tena unasema mumeo anakupenda. Hata hivyo, iwapo unaamini hali hiyo haitabadilka ni muhimu ufungue moyo wako kwake umwambie ukweli ili ajue la kufanya.

Nikishaonja tu basi sina hamu naye tena

Shangazi natumai wewe ni mzima. Naomba unipe ushauri kuhusu jambo moja ambalo linanisumbua. Kila nikipendana na mwanamume kisha turushe roho mimi humchukia na huwa hata sitaki kumuona tena. Ni kwa nini? Kupitia SMS

Hizo ni dalili za mapenzi yasiyo ya dhati. Nahisi kuwa umekuwa ukiongozwa na hisia za mwili wala si za moyoni na ndiyo maana zikishughulikiwa huwa ni basi huna haja tena. Mapenzi kutoka moyoni hudumu hata hisia za mwilini zikitoweka. Ni mapenzi ya dhati tu yatakayokutoa katika hali hiyo.

Dadaye hataki anioe eti ninamzidi umri

Shikamoo shangazi. Nina mpenzi ambaye tumepanga kuoana ingawa amenizidi umri kwa miaka mitatu. Lakini dada yake amekuwa akipinga uhusiano wetu kwa sababu ya tofauti hiyo ya umri akidai tunapotezeana wakati. Nishauri. Kupitia SMS

Uhusiano wenu haumhusu sikio wala ndewe huyo dada ya mpenzi wako. Kama hakuna kati yenu anayetatizwa na hiyo tofauti fungeni masikio na muendelee na mipango yenu. Inawezekana huyo dada yake anawaonea wivu.

Mume aliyeoa tayari amenitia mimba, sijui nifanye nini

Nina umri wa miaka 20 na nimependana na mwanamume ambaye ana mke na nimepata mimba yake. Alikuwa ameahidi kunioa lakini wazazi wangu hawataniruhusu. Nifanyeje? Kupitia SMS

Hapo umefanya makossa mara mbili. Kosa la kwanza ni kuwa na uhusiano na mwanaume ambaye ana mke. La pili ni kukubali kubeba mimba yake nab ado hajakuoa. Kama wazazi wako wamekataa ukiolewa mke wa pili itabidi uwe tayari kulea mtoto hadi utakapopata mume.

Binti huyu anasema niwe wake wa pili

Vipi shangazi? Kuna msichana ambaye amekuwa akinitembelea kwangu na sijui nia yake hasa. Nilimuuliza iwapo ana mpenzi akasema anaye lakini hangejali kuwa na wawili. Nahisi kuwa ananipenda lakini hataki kuniambia. Nishauri. Kupitia SMS

Inaonekana msichana huyo amekuwa akikutaka na ameamua kwamba ni lazima ujue. Huenda hata hana mwingine na anatafuta tu hakikisho kutoka kwako kuwa wewe pia unampenda. Fuatilia ujue kama ana mwingine ili upate mwelekeo.

Japo amesoma sana, ataka niache shule eti ndipo anioe mimi

Vipi shangazi. Mimi ni mwanafunzi wa shule ya upili na nimependana na mwanamume msomi na mwenye maendeleo maishani. Ajabu ni kuwa anataka niache shule anioe na ametishia kuwa kama sitaki atatafuta mwingine. Sitaki kumuacha na pia nathamini masomo. Nishauri tafadhali. Kupitia SMS

Mapenzi yanaweza kukupumbaza ukose kuona wala kusikia na nahisi yamekufika hapo. Kumbuka kuwa anayekwambia uache shule tayari amemaliza masomo na yuko sawa maishani. Ndoa si haina mikataba, anaweza kukuoa na baadaye akuache. Itakuwaje? Jenga msingi wa maisha yako kwanza, mengine baadaye.

Nina miaka 24 lakini sina mpenzi, sijui nifanye nini, saidieni

Shangazi shikamoo. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka na 24 sina mpenzi. Natamani sana kuwa na kwangu. Nishauri. Kupitia SMS

Mapenzi si maji, hayachotwi mtoni. Ni lazima kwanza watu waonane na wapendane ndipo wawe wapenzi. Utaratibu huo unaweza kuchukua muda mrefu na itabidi uwe na subira. Isitoshe, wewe bado ni mchanga na huna haja ya kuwa na wasiwasi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.