Consolata kwaheri

Taifa Leo - - SOKOMOKO -

Mama nakumbuka sana, upendo ulotwonyesha,

Ni pigo kwa sote wana, kukukosa kwa maisha,

Mauti wewe hiana, mametu mesafirisha, Lala salama mamangu, Bi Consolata kwaheri.

Taswirazo zingalipo, hazitoki karibuni, Tulia papo ulipo, najua uko peponi, Maisha haya upepo, mametu twakutamani, Lala salama mamangu, Bi Consolata kwaheri.

Kukukosa ni uchungu, uchungu usosemeka,

Ila twamuomba Mungu, subira atatuvika, Yalotufika machungu, nyoyoni twataabika, Lala salama mamangu, Bi Consolata kwaheri.

Ndugu zangu jikazeni, kipindi hiki kigumu, Atupe subra Manani, kaziye tusilaumu, Ingawa huu mtihani, kuupita ndo muhimu, Lala salama mamangu, Bi Consolata kwaheri. FRANCIS MAINA MACHARIA ‘Bin Macharia’ Kisauni, Mombasa

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.