Domo domo tuliache

Taifa Leo - - SOKOMOKO -

Vijana kwenu nanena, tuliache domodomo, Tufanye kazi ya maana, vijijini kwetu humo, Tufaane kwa mapana, kuliko kupiga domo, Siasa isije tuponza, tupoteze mwelekeo.

Inapofika macheo, kiguu na njia waenda, Ni siasa hadi machweo, barabarani washinda, Watetea wenye vyeo, huku mwenyewe wakonda,

Siasa isije tuponza, tupoteze mwelekeo.

Uchaguzi ni musimu, hivi utakuja kwisha, Ubaki kujilaumu, njaa itakapobisha, Wenzako tukijikimu, kwa zao tulozalisha, Siasa isije tuponza, tupoteze mwelekeo.

Mesahau hata dini, mikutano kila mara, Mwafanya juu na chini, mwaifwata misafara, Mumekwisha futa dini, katika zenu shajara, Siasa isije tuponza, tupoteze mwelekeo.

Leo wapewa vipeni, waiacha yako kazi, Waabudu kampeni, kuliko Mungu Mwenyezi, Wewe binadamu gani, kufanya kazi huwezi, Siasa isije tuponza, tupoteze mwelekeo.

AYIEKO JAKOYO ‘Malenga wa Bara’

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.