Laleni pema

Taifa Leo - - SOKOMOKO -

Kono linatetemeka, na macho yarowa rovu, Moyoni ninavunjika, wamenitonesha kovu, Hativo nalazimika, kutaja huno uovu, Vijana laleni pema, Maulana talipiza.

Wasichana nguzo yetu, hasa wale wasomao, Huyu alokosa utu, hakuona kazi yao? Alojifanya ni jitu, kumaliza nafsi zao,

Vijana laleni pema, Maulana talipiza.

Karo iliyotumika, imezama majivuni, Maono yalotajika, yameishiya motoni, Hawawezi sahulika, inatibua mtimani, Vijana laleni pema, Maulana talipiza.

Ngeu sasa yaniganda, wana Moi dato mosi, Walokuwa wakipanda, elimu wamguse tosi, Sasa ona wanavunda, hawana tena nafasi, Vijana laleni pema, Maulana talipiza.

Waumini kanisani, pamoja na msikitini, Tuwatie maombini, tukiswali twatajeni, Naondoka ukumbini, na fundo kubwa moyoni, Vijana laleni pema, Maulana talipiza.

AVAGWA TITUS ARONYA

Kawangware

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.