Amani tuitaraji

Taifa Leo - - SOKOMOKO -

Wa miji mnaoranga, kuhangaika na jiji, Matulivu kujipanga, wana wa Kenya wa miji, Tujiepushe majanga, tusionyane ugwiji, Amani tujifariji, pasi ncha ya upanga.

Tupulizeni kipenga, Wanakenya wakaaji, Malengo yetu kulenga, lekezo malekezaji, Tujenge nchi kujenga, Kenya moja mahitaji, Amani twaitaraji, pasi ncha ya upanga.

Tujenge nchi kuganga, kimajenzi ujengaji, Miradi kuifinyanga, tusiwe wachafuwaji, Wa uchumi kubananga, pambi pambo upambaji,

Amani udumishaji, pasi ncha ya upanga.

Tusibebe masharanga, na nyuta za mafumaji, Tusicharane mapanga, damu damu umwagaji, Tujitolee muhanga, amani kudumishaji, Yeenezee wenezaji, pasi ncha ya upanga. ABDALLA SHAMTE ‘Mtumwa wa Mungu’ Mwembekuku, Mombasa

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.