Fahali mkipigana

Taifa Leo - - SOKOMOKO -

Alfajiri twaamka, macheo yametujia, Umande unanyauka, jua linatufikia, Zizi linapofunguka, kwato zinatupitia, Fahali mkipigana, sisi nyasi twaumia.

Shamba la mtu mmoja, jina lake mkulima, Na hiyo plau ni moja, mwakokota mkilima, Malishoni ni pamoja, mbona mwala kijipima? Fahali mkipigana, sisi nyasi twaumia,

Hatuelewi kwa nini, mkulima katupanda, Maisha yetu ya chini, tunaliwa nao punda, Nayo miti ya majani, hivi mbona kutopanda? Fahali mkipigana, sisi nyasi twaumia.

Kwato mwaziparagaza, nalo vumbi mwalitifua, Mie mnanikwaruza, huku mwapiga vifua, Maishangu gandamiza, ninakosa kupumua, Fahali mkipigana, sisi nyasi twaumia.

USTADH MISIKO JOHN ‘Malenga wa Magharibi’ Nairobi

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.