Starlets yajikatia tikiti nusu fainali kombe la COSAFA

Warembo wa Kenya wadhalilisha Mauritius 11-0

Taifa Leo - - SPOTI - Na GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Starlets ya Kenya iliifunza Mauritius jinsi ya kutandaza soka baada ya kuibwaga 11-0 na kunasa tiketi ya nusu-fainali katika mashindano ya Afrika ya Kusini (COSAFA) mjini Bulawayo nchini Zimbabwe jana.

Viongozi hao wa kundi B walipata mabao yao kupitia Neddy Atieno (manne), Mwanahalima Adam na Lucy Mukhwana (mabao mawili kila mmoja) nao Cheris Avilia na Dorcas Sikobe wakachangia bao moja kila mmoja. Starlets ya kocha Richard Kanyi pia ilinufaika kufungiwa bao moja na mchezaji wa Mauritius M. Rassoie dakika ya 90. Kufikia sasa, ushindi huu ni mkubwa kabisa katika mashindano haya.

Kenya ilichukua uongozi dakika ya tisa baada ya Adam kukamilisha pasi safi ya Wendy-ann Achieng’.

Bao lake la pili

Atieno aliimarisha uongozi huo dakika ya 25 kabla ya kupata bao lake la pili dakika ya 32.

Mukhwana alifanya mambo kuwa 4-0 dakika mbili baadaye kabla ya Atieno kupachika bao lake la tatu la mechi na la sita mashindanoni dakika za majeruhi za kipindi cha kwanza.

Kenya ilifanya mabadiliko matatu mapema katika kipindi cha pili ikijaza nafasi za Achieng’, ambaye alipata kadi ya njano dakika ya 29, Pauline Msungu na Carolyne Omondi na wachezaji Cheris Avilia, Lilian Adera na Florence Awino.

Mukhwana alisukuma wavuni bao la sita dakika ya 49 baada ya kupata pasi kutoka kwa Atieno, ambaye aliongeza la saba dakika mbili baadaye.

Atieno alimega pasi iliyozalisha bao la nane lilofungwa na Avilia dakika ya 54 kabla ya Sikobe kufanya mambo kuwa 9-0 dakika ya 79 baada ya kupata pasi kutoka kwa Adam, ambaye aliona lango tena dakika ya 85. Rassoie alijifunga dakika ya 92.

Kenya ilitumia ujuzi wake wa Kombe la Afrika (AWCON 2016) kuiponda Mauritius kisawasawa. Wachezaji wa Kenya walioshiriki AWCON nchini Cameroon na ambao wanapeperusha bendera nchini Zimbabwe ni Lilian Adera, Avilia, Omondi, Achieng’ na Sikobe.

Mechi ya mwisho ya makundi ya Kenya ni dhidi ya Swaziland hapo kesho. Starlets ilianza kampeni yake kwa kunyamazisha Msumbiji 5-2 mnamo Septemba 14. Atieno alifunga mabao matatu katika mechi hiyo, huku Adam na Phoebe Owiti wakichangia bao moja kila mmoja.

Wakenya wanashiriki mashindano haya ya mataifa 12 kwa mwaliko kutoka Shirikisho la Soka la Afrika ya Kusini (COSAFA). Mataifa mengine yanayoshiriki ni Afrika Kusini, Lesotho, Namibia na Botswana ambayo yanajumuisha kundi C. Zimbabwe, Zambia, Malawi na Madagascar yalitiwa katika kundi A. Afrika Kusini inajivunia mataji ya mwaka 2002, 2006 na 2008. Zimbabwe ilishinda makala ya mwaka 2011. Ilipiga Afrika Kusini 1-0 katika fainali. Mashindano haya yanarejea baada ya kutofanyika miaka mitano mfululizo. Baadhi ya mataifa ambayo yameonyesha dalili za kutwaa ubingwa kufikia sasa ni Afrika Kusini, Zimbabwe, Zambia, Namibia na Kenya. Wageni Kenya watapumzika leo.

Hata hivyo, Zambia itachuana na Madagascar, Namibia ilimane na Lesotho, Zimbabwe ikabane koo na Malawi nayo Afrika Kusini ilikabiliane na Botswana. Mashindano haya yatakamilika Septemba 24.

Picha/maktaba

Golikipa wa Harambee Starlets Pauline Atieno wakati wa mazoezi kabla ya dimba la Cosafa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.