Lionesses yaadhibu Senegal, Madagascar

Taifa Leo - - SPOTI - Na GEOFFREY ANENE

KENYA iliponda Madagascar 27-5 na Senegal 38-0 na kujinasia tiketi ya nusu-fainali katika Kombe la Afrika la raga ya wachezaji saba kila upande la wanawake nchini Tunisia jana.

Lionesses ya kocha Kevin Wambua, ambayo ilifika fainali za mwaka 2014, 2015 na 2016, sasa inajivunia ushindi mara tano mfululizo dhidi ya Madagascar.

Kenya ilizima Madagascar 29-10 mwaka 2011, 24-14 mwaka 2014, 33-0 mwaka 2015 na 38-0 (2016).

Haijapata dawa

Senegal pia haijapata dawa ya kupata sare ama ushindi dhidi ya Kenya. Baada ya kupepetwa 22-0 mwaka 2014 na 52-0 mwaka 2015 na Kenya, Senegal ilizidiwa maarifa tena. Kasi ya wachezaji wa Kenya akiwemo nyota Janet Okello, ilitatiza wapinzani wake sana.

Lionesses ilipangiwa kukamilisha mechi zake za makundi dhidi ya Zimbabwe jana jioni ikitafuta kulinda rekodi yake ya kutoshindwa na Wazimbabwe hadi mechi tatu. Katika mechi za awali kati ya mataifa haya, Kenya ilizima Zimbabwe 39-0 katika nusu-fainali ya mwaka 2015 na kuilemea tena 31-5 katika nusu-fainali mwaka 2016.

Kenya ilipoteza dhidi ya Afrika Kusini katika fainali za mwaka 2014, 2015 na 2016. Ililimwa 1410 mwaka 2014, 31-5 (2015) na 22-17 (2016).

Mashindano haya ambayo yameleta pamoja mataifa manane yatakamilika leo. Bingwa wa Afrika atafuzu kushiriki Kombe la Dunia litakaloandaliwa na Marekani mjini San Francisco mnamo Julai 20-21 mwaka 2018. Kufikia sasa, mataifa 10 yamefuzu kushiriki kombe hilo. Mataifa hayo ni Marekani, Canada, Uhispania, Ufaransa, Urusi, Uingereza, Ireland, New Zealand, Australia na Fiji.

Makundi ya Kombe la Afrika (2017): A – Afrika Kusini, Uganda, Tunisia, Morocco; B – Kenya, Zimbabwe, Senegal, Madagascar.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.