SIUNGI SHERIA MPYA -CHEBUKATI

Kinara wa IEBC asema uchaguzi ujao utaendeshwa chini ya sheria zilizopo

Taifa Leo - - FRONT PAGE - Na WYCLIFFE MUIA

MWENYEKITI wa Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC) Wafula Chebukati jana alipuuzilia mbali njama ya Jubilee ya kubadilisha sheria za uchaguzi akisema marudio ya uchaguzi wa Oktoba 26 hayahitaji sheria mpya.

Bw Chebukati alisema japo hana mamlaka ya kuingilia wajibu wa Bunge, ni vyema pande zote husika kujadiliana pamoja badala ya kuzua utata wa kubadilisha sheria za uchaguzi.

Mwenyekiti huyo alisema yeye au kamishna yeyote wa tume hiyo hahitaji mamlaka zaidi mbali na waliyopewa na katiba.

“Uamuzi wa Mahakama ya Juu haukulaumu sheria kwa makosa yaliyopelekea kufutiliwa mbali kwa uchaguzi wa urais. Kile ambacho mahakama ililaumu ni mikakati ndani ya IEBC ambayo tunaendelea kulainisha,” alisema Bw Chebukati.

Mwenyekiti huyo alisema hayo baada ya mazungumzo yaliyoongozwa na tume hiyo katika ukumbi wa Bomas kati ya chama cha Jubilee na muungano wa NASA kutibuka tena kuhusiana na hatua ya Jubilee kuanzisha rasmi mchakato wa kubadilisha sheria za uchaguzi kupitia bunge.

Bw Chebukati alisema tume hiyo inaendelea kutathmini mabadiliko hayo ya sheria na kuelezea matumaini ya IEBC kuwa hayataathiri uchaguzi wa Oktoba 26 iwapo yatapitishwa na bunge.

“Japo mkutano na wadau wakuu umetibuka, uchaguzi bado utafanyika Oktoba 26 lakini tutaendelea kuwafikia wawaniaji wa urais ili kusuluhisha masuala tata,” akasema.

Mwenyekiti huyo alisema tume hiyo kamwe haitakubali wawaniaji wa urais kuwakilishwa na maajenti wao wa kisiasa katika mkutano ujao.

“Masuala ambayo NASA inataka yashughulikiwe kabla ya uchaguzi si nyeti sana na iwapo tutapatana na vinara wawili binafsi wa pande zote, itakuwa rahisi sana kuyatatua,” alisema Bw Chebukati aliyeandamana na kamishna Paul Kurgat.

Ujumbe wa NASA ulioongozwa na Seneta wa Siaya James Orengo uliondoka kikaoni dakika chache baada ya kuanza ukilalamikia njama ya Jubilee kutaka kuingilia mamlaka ya IEBC kwa kutumia idadi yake kubwa ya wabunge. Pande zote zilithibitisha kuwa hakuna ajenda hata moja iliyosuluhishwa katika mkutano wa jana.

“Sheria wanazotaka kubadilishwa ziliundwa na wawakilishi wa Jubilee wa NASA ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unaaminika na wadau wote. Tulikubaliana hakuna kubadilisha sheria hizo lakini inaonekana Jubilee wanataka kujaribu ustahimilivu wa Wakenya. Chochote kitakachotokea baadaye Jubilee sharti iwajibikie,” alisema Bw Orengo.

Wakili huyo alisema Jubilee inalenga kupunguza mamlaka ya mwenyekiti wa IEBC ili kuhakikisha kuwa kamishna yeyote ana uwezo wa kutangaza matokeo ya urais, iwapo mwenyekiti hayupo.

“Jubilee inataka kugeuza IEBC kuwa bwege lakini kile ningetaka kuwaambia ni kuwa wao ndio watakaokuwa washinde kwa sababu hakuna uchaguzi utakaofanyika nchini ya hayo mabadiliko,” akasema.

“Uamuzi wa mahakama uliamuru IEBC irudie uchaguzi wa urais kwa kufuata sheria na wala si kubadilisha sheria... sasa wanataka kurudia wizi wa kura kwa kubadilisha sheria,” akasema Bw Orengo ambaye alikuwa ameandamana na Afisa Mkuu Mtendaji wa NASA Norman Magaya na wakili Paul Mwangi. Habari zaidi Uk 3, 5

Picha/jeff Angote

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (IEBC), Wafula Chebukati (kulia) pamoja na Paul Kurgat wahutubia wanahabari katika ukumbi wa Bomas of Kenya wakati wa mkutano wa mashauriano baina ya muungano wa Nasa na chama cha Jubilee jana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.