Ruto aonya kuwa maandamano yanaweza kuzua ghasia

Taifa Leo - - FRONT PAGE - TITUS OTEBA na VALENTINE OBARA

SIASA

NAIBU wa Rais, William Ruto, jana alionya viongozi wa Muungano wa NASA dhidi ya kuandamana.

Kulingana na Bw Ruto, maandamano yatasababisha mandhari ya ghasia sawa na zilizotokea baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007.

Akizungumza katika kijiji cha Namwacha kilicho eneobunge la Kanduyi, Kaunti ya Bungoma, Bw Ruto alisema hawataruhusu Kiongozi wa NASA, Bw Raila Odinga na wenzake kuendelea kumtishia Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati na Afisa Mkuu Mtendaji Bw Ezra Chiloba.

“Kama Raila anataka uchaguzi kweli, ni bora ashindane na wenzake kwenye uchaguzi na akome kubishana na vijana wadogo kama Chiloba,” akasema.

Alikuwa ameandamana na viongozi kadhaa wa eneo hilo ambapo alitoa ahadi tele za maendeleo huku akiahidi kwamba Jubilee ikishinda urais itakamilisha miradi mingine iliyokuwa imeanzishwa.

Jana, Bw Odinga alisisitiza kuwa wataendelea na maandamano yao ingawa yataanza Jumatatu wiki ijayo, na yatakuwa yakifanywa kila Jumatatu na Ijumaa hadi masharti yao kuhusu maandalizi ya uchaguzi wa urais wa marudio yatimizwe.

Kulingana na Bw Odinga, Jubilee ilidhihirisha kuwa haina nia ya kupata maelewano kuhusu maandalizi hayo ilipowasilisha hoja bungeni kubadilisha sheria za uchaguzi wakati ambapo mashauriano yalikuwa yakiendelea kati ya pande hizo mbili na makamishna wa IEBC.

Akizungumza katika kikao cha wanahabari Nairobi, Bw Odinga alisema NASA ilionyesha nia njema ilipokubali mashauriano kabla ya uchaguzi uliopita ambayo yalifanya sheria za uchaguzi kubadilishwa kwa njia iliyokubalika na wadau wote.

Kulingana naye, maandamano yao yatalenga kupinga juhudi za Jubilee kutumia wingi wao bungeni kwa maslahi ya kibinafsi, mbali na kutaka baadhi ya maafisa wa IEBC wasimamishwe kazi kabla uchaguzi ufanywe.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.