SIASA: VIONGOZI WA NASA SASA KUPEWA MLINZI MMOJA MMOJA KILA MMOJA

Taarifa ya Polisi yasema walinzi walioondolewa wamepewa majukumu mengine

Taifa Leo - - FRONT PAGE - Na BERNARDINE MUTANU

VIONGOZI wa upinzani, NASA, wamebakiziwa mlinzi mmoja pekee baada ya Idara ya Polisi kuwaagiza maafisa wa polisi wanaowalinda kupewa majukumu mengine.

Viongozi hao walibakiziwa mlinzi mmoja wa kibinafsi na mmoja wa nyumbani.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari kutoka kwa Idara ya Polisi na iliyoandikwa Septemba 25 kwa niaba ya Naibu Inspekta wa Polisi na Bw Benson Kibue, maafisa wote wa polisi ambao ni walinzi wa viongozi wa awali wanahitajika kurejelea majukumu yao ya kawaida.

“Kutokana na upungufu wa maafisa wa polisi katika kutoa huduma kwa umma na kutokana na ongezeko la mahitaji kwa sababu ya changamoto zilizoongezeka, imekuwa muhimu kuchukua hatua,” barua hiyo iliyoandikiwa makamanda wa polisi katika maeneo ya kaunti imesema.

Pia, viongozi waliopoteza katika uchaguzi mkuu uliopita wakiwemo maseneta na wabunge wameathiriwa katika hatua hiyo.

“Tunawaamrisha maafisa wote wa kutoa ulinzi kwa wabunge wa awali na maseneta pamoja na wale wa waziri mkuu wa zamani, aliyekuwa makamu wa rais na aliyekuwa naibu wa waziri mkuu kurudi,” ilisema taarifa hiyo.

Iliongeza kuwa Mabw Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi watasalia na mlinzi mmoja pekee wa kibinafsi, na mmoja wa kudumisha usalama nyumbani mwao nyakati za usiku peke yake.

Hii inamaanisha kuwa wabunge na maseneta wa awali watabakiziwa mlinzi mmoja kuambatana na amri hiyo.

Wakenya wote walio na walinzi wa serikali ambao hawakuidhinishwa na kamati ya kitaifa ya ushauri wa usalama (NSAC) ila wale walio na idhini ya moja kwa moja kutoka kwa Huduma ya Polisi pia wamepokonywa walinzi kulingana na agizo hilo.

NSAC imesimamiwa na Rais na wanachama wengine ni naibu wa rais, waziri wa ulinzi, waziri wa usalama wa ndani, waziri wa mashauri ya kigeni, mwanasheria mkuu, msimamizi wa jeshi, mkurugenzi mkuu wa Idara ya Ujasusi na Inspekta Mkuu wa Polisi.

Kulingana na taarifa hiyo, maafisa wa kutoa ulinzi katika majumba ya kibinafsi kama vile mabenki pia watapunguzwa, “kuhakikisha kuwa maafisa wetu wanatekeleza majukumu ya lazima na muhimu.”

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.