Jubilee yapitisha hoja mbili tata bungeni kubadilisha sheria

Mabadiliko haya sheria za uchaguzi yanapingwa na NASA

Taifa Leo - - FRONT PAGE - Na LUCY KILALO

WABUNGE wa chama cha Jubilee jana walianza harakati za kubadilisha sheria za uchaguzi baada ya hoja mbili zinazonuia kutekeleza mabadiliko hayo kusomwa kwa mara ya kwanza bungeni.

Hatua hiyo ilijiri baada ya wabunge hao kupitisha hoja ya kupunguza muda wa kuchapishwa kwa Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi, na Marekebisho ya Sheria ya Makosa ya Uchaguzi, ambayo itaelekeza jinsi uchaguzi wa urais utakavyoendeshwa.

Lakini hoja hiyo ya kupunguza muda huo, ilipingwa na wabunge wa Muungano wa NASA pamoja na marekebisho yanayopendekezwa kwa Sheria ya Uchaguzi, wakisema kuwa haistahili kwa sasa kwa kuwa IEBC inastahili kuendesha uchaguzi kulingana na maagizo ya Mahakama ya Juu. Muungano huo ulisema hautajihusisha na mabadiliko hayo.

Kiongozi wa Walio Wengi Bungeni, Bw Aden Duale alipendekeza muda wa kuchapishwa kwa Sheria ya Makosa ya Uchaguzi, inayotoa adhabu kwa maafisa wa uchaguzi watakaoenda kinyume na taratibu, na Sheria ya Uchaguzi upunguzwe kutoka siku 14 hadi siku moja, kwa kuwa hakuna muda hasa ikizingatiwa kuwa uchaguzi wa urais unatarajiwa kufanyika Oktoba 26.

“Mswada unarekebisha mambo yaliyotajwa na uamuzi huo. Mswada utatuliza joto lililopo nchini na kutuleta pamoja, kwa kuwa biashara zinatatizika, nchi imegawanyika. Hakuna jambo lolote la “utundu” katika mswada huu. Tunamheshimu Jaji Maraga na majaji wote sita. Lakini tunataka IEBC iwe na uhakika kabisa inapoendesha uchaguzi huu,” Bw Duale aliambia Bunge.

Lakini akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Rarieda, Bw Otiende Amollo alipuuzilia mbali marekebisho hayo akisema ni kinyume cha sheria na huenda yakaibua changamoto zaidi kuhusiana na uchaguzi unaotarajiwa.

“Hata tufanye nini, tukipitisha hoja hii bado itakuwa kinyume cha sheria na huenda tukaishia kuahirisha uchaguzi kutoka Oktoba 26 hadi tarehe isiyojulikana,” alisema.

Alisema kuwa Mahakama ya Juu ilifanya uamuzi wake kwamba uchaguzi lazima uendeshwe kulingana na Katiba ya sasa kama ilivyokuwa Agosti 8 uchaguzi ulipofanyika.

Mbunge wa Kiminini, Dkt Chris Wamalwa pia alipinga hoja hiyo akisema kuwa siku 14 ni muhimu kwa matayarisho na hata kuweza kushirikisha umma.

“Unaporekebisha sheria lazima ulete na kanuni za kuiwezesha kutekelezwa. IEBC italazimika kuunda kanuni hizo, na hatuna muda,” alieleza.

Bw Duale alipinga madai kuwa mswada huo unalenga kudhibiti mamlaka ya Mahakama ya Juu hasa baada ya uamuzi wake wa kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 8.

Kamati teule ya wabunge tisa wa Jubilee ndiyo inayotarajiwa kuongoza marekebisho hayo. Mwenyekiti wa kamati hiyo, ni Bw William Cheptumo. Wanakamati wengine ni Bi Gladys Shollei, Bw Isaac Ndirangu, Bw Ali Wario, Bi Jennifer Shamalla, Bw Adan Yusuf, Bw George Murugura, Bw Stanley Muthama na Bi Ali Wahome.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.