Mahakama yakataa ombi la Karua

Taifa Leo - - NEWS - Na GEORGE MUNENE

OMBI la kiongozi wa chama cha Narc Kenya Bi Martha Karua la kutaka kesi aliyowasilisha kupinga uchaguzi wa Gavana Anne Waiguru isikilizwe na Majaji watatu wa Mahakama Kuu lilitupiliwa mbali.

Jaji Lucy Gitari wa Mahakama Kuu ya Kerugoya alisema kesi hiyo ya kuomba korti iharamishe uchaguzi wa Bi Waiguru yapasa kusikilizwa na jaji mmoja tu.

“Kesi hii haijazua masuala mazito ya kisheria na kikatiba ambayo hayawezi kuamuliwa na jaji mmoja,” alisema Jaji Gitari.

Jaji huyo alisema aliteuliwa na Jaji Mkuu (CJ) David Maraga kusikiliza na kuamua kesi hiyo ya kupinga uchaguzi wa Gavana Waiguru aliyemshinda kinara huyo wa Narc Kenya kwa wingi wa kura.

Jaji huyo aliorodhesha Oktoba 4 kuwa siku ya kuanza kusikilizwa kwa kesi ya kuharamisha ushindi wa Bi Waiguru.

Bi Waiguru alizoa kura 161,373 ilhali Bi Karua alifaulu kupata kura 122,091.

Katika ombi lake, Bi Karua alisema kesi yake inazua masuala mazito ya kisheria yanayoweza kuamuliwa tu na Majaji watatu watakaoteuliwa na CJ.

Mahakama ilifahamishwa kwamba sheria za uchaguzi zilikiukwa na kwamba wizi ulikithiri na wapigakura kupewa milungula.

“Mahakama hii imeteuliwa na CJ kusikiliza na kuamua kesi hii ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Gavana Waiguru. Nitaisikiliza pasi na woga wala upendeleo,”alisema Jaji Gitari.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.