Wakazi walalamikia kukatizwa huduma za feri

Taifa Leo - - NEWS - Na HAMISI NGOWA

WAKAZI wa Mtongwe eneobunge la Likoni jana waliandamana hadi kwenye ofisi za Shirika la Huduma za Feri, [KFS] wakilalamikia kukosekana kwa huduma za feri katika kivuko cha Mtongwe.

Wakazi hao waliokuwa wamebeba matawi, walipiga kambi nje ya ofisi za shirika hilo wakitaka kuelezwa sababu za kukatizwa kwa huduma za uchukuzi wa feri katika kivuko hicho.

Wakiongozwa na msemaji wao Micheal Ogwambo, walidai kuwa kumekuwepo na ukosefu wa huduma za feri katika kivuko hicho kwa kipindi cha majuma mawili.

“Tunaona ni kama kurejeshwa kwa huduma za feri katika kivuko cha Mtongwe zilikuwa mbinu ya kutafuta siasa kwa sababu tangu kukamilka kwa uchaguzi mwezi Agosti, huduma hizo zimekuwa hazitolewi jinsi zilivyoratibiwa,” akasema.

Alisema kumekuwa na hali ya kukatizwa kwa huduma hizo pasi kutolewa ilani ya kuarifu abiria wanaotumia kivuko hicho.

Lakini akizungumza na wanahabari, afisa wa shirika hilo anayeshughulikia maslahi ya wateja, Bw Francis Mgomati, aliwahakikishia watumizi wa kivuko cha Mtongwe kwamba huduma katika kivuko zitarejelewa Jumamatu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.