Katibu Mkuu El Maawy aliyeuawa na Shabaab kuzikwa leo

Taifa Leo - - HABARI ZA KAUNTI - KALUME KAZUNGU na MOHAMED AHMED

ALIYEKUWA katibu mkuu wa masuala ya ujenzi Maryam El Maawy aliyefariki Afrika Kusini baada ya kushambuliwa na wanamgambo wa Al-shabaab miezi miwili iliyopita atazikwa leo.

Bi El Maawy alipata majeraha mabaya baada ya shambulizi hilo la Julai 13 na alipelekwa katika hospitali ya Milpark jijini Johannesburg ambapo alifariki. Kulingana na msemaji wa familia yao, Bw Mohammed Ali, marehemu atazikwa baada ya swala ya Ijumaa katika msikiti wa South C.

“Atazikwa katika makaburi ya Lang’ata. Saa hii tunaelekea Nairobi kwenda kupokea mwili wake katika uwanja wa ndege wa JKIA na tupange mazishi hayo,” akasema Bw Ali.

Alisema Bi El Maawy alikuwa amekaa takriban miezi miwili nchini Afrika Kusini akitibiwa, kabla ya kufikwa na mauti mnamo Jumatano.

Jana katika kaunti ya Lamu ambako ni asili ya katibu huyo, wakazi walijawa na majonzi habari za kifo chake zilipoenea, huku zikitangazwa hata kupitia misikiti.

Viongozi wa kidini msikitini walimsifu Bi El Maawy kuwa kiongozi ambaye alikuwa mfano bora kwa watu wa Lamu.

Akizungumza na Taifa Leo ofisini mwake jana, Gavana Fahim Twaha alimtaja Bi El Maawy kuwa mfano bora hasa kwa jinsia ya kike Lamu, kutokana na usomi wake.

“Alikuwa kiongozi aliyejitolea kuitumikia serikali. Alikuwa kielelezo bora kwa wasichana wetu hapa Lamu. Kifo chake ni pigo kwa jamii nzima ya Lamu,” akasema Bw Twaha.

Aliitaka serikali iimarishe usalama Lamu, hasa dhidi ya kundi la Al-shabaab.

Aliyekuwa Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Lamu, Bi Shakila Abdalla, alitaja kifo cha Bi El Maawy kuwa doa jeusi kwa Lamu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.