Mbunge wa ODM adai Kamishna ana njama ya kumuua

Taifa Leo - - HABARI ZA KAUNTI - Na LUCY KILALO

MBUNGE wa Kajiado Kati Elijah Memusi amemtaka kaimu Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i kuchunguza vitisho anavyopokea kutoka kwa Kamishna wa Kaunti ya Kajiado, akidai kuwa amepokea taarifa mkuu huyo ametuma watu kumwangamiza.

Bw Memusi alisema kuwa kamishna huyo, Bw Kello Harsama hata anahitaji kuhamishwa uchunguzi huo ukiendelea ama watamtimua kwa lazima.

“Nilipokea habari kuwa kamishna wa kaunti Kello Harsama amenitumia wauaji. Jumatatu nilitoa taatifa kuhusu Bw Harsama kwa kutumia afisi yake vibaya. Kello Warsama amekuwa Kajiado kwa zaidi ya miaka 15, amekaa sana na kutumia afisi yake kujitajirisha na amenyakua ardhi, na Jumatatu nilimfichua. Jumanne nasikia aliitisha mkutano ambapo aliagiza afisa kuniandama Nairobi na anipige risasi,” mbunge huyo alieleza wanahabari jana nje ya kituo cha polisi cha Bunge akieleza kuwa habari hizo tayari ziko na polisi na angependa wazichunguze.

“Sitatishwa na yeyote. Nitaendelea kukabiliana na mtu yeyote anayetaka kuwatumia vibaya watu wangu wa Kajiado ya Kati,” alisema akiwa ameandamana wabunge wenzake wa muungano wa NASA. Seneta Maalum, Judy Pareno alisema kuwa kamishna huyo atalazimika kuwajibika iwapo lolote litamfanyikia mbunge huyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.