Wafuasi wa Babu Owino wazuia polisi kumkamata

Wakataa kuondoka kortini Kibera baada ya mbunge huyo kuachiliwa

Taifa Leo - - HABARI ZA KAUNTI - BENSON MATHEKA na R. MUNGUTI

WAFUASI wa mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, jana walizima juhudi za polisi za kutaka kumkamata alipoachiliwa kwa dhamana na mahakama ya Kibera.

Wafuasi hao walikataa kuondoka ndani ya mahakama iliyojaa maafisa wa polisi, ambao mawakili wa mbunge huyo walisema walikuwa na maagizo ya kumkamata tena.

Hakimu Mkuu Joyce Gandani alikataa ombi la upande wa mashtaka la kumnyima dhamana na kuonya kwamba Wakenya wanatazama jinsi serikali inavyotumia mfumo wa sheria kuhangaisha upinzani.

Wakiongozwa na wabunge Kenn Okoth, Millie Odhiambo, Otiende Amollo na James Orengo wafuasi hao waliosindikiza Babu wakiimba nyimbo za kumsifu hadi nje ya Mahakama na kutembea kwa miguu kuelekea mtaa wa Ayany.

Wakati mmoja polisi walirusha hewa ya kutoa machozi lakini wafuasi hawakutishika.

Awali asubuhi, mbunge huyo alishtakiwa kuwa Bw Owino, ambaye majina yake kamili ni Paul Ongili, alimpiga Bw Joshua Otieno Obiende katika kituo cha kupigia kura cha Soweto mnamo Agosti 8.

Shtaka la pili ni kuwa alikiuka sheria za uchaguzi kwa kutumia nguvu kumzuia Bw Obiende aliyekuwa mgombeaji wa chama cha Amani National Congress (ANC) nafasi ya kupiga kura.

Alikanusha mashtaka yote na kuhusisha masaibu yake na kesi ya kupinga ushindi wake kama mbunge.

“Lengo la kesi hii na nyingine ambazo mshtakiwa amesingiziwa ni kuhakikisha amepoteza kiti chake cha ubunge na kuzuiwa kugombea wadhifa wowote wa umma,” alisema wakili wake Bw Amollo.

Alisema Bw Obiende ni malalamishi katika kesi ya kupinga ushindi wa Bw Owino.

Kiongozi wa mashtaka Nicholas Mutuku alipinga ombi akisema mbunge huyo anachunguzwa na Tume ya Maadili na Kupambana na ufisadi (EACC).

“Mshtakiwa anachunguzwa kwa mujibu wa kifungu cha sita kuhusu Maadili ya viongozi,” alisema Bw Mutuku.

Alisema mbunge huyo anaweza kuwatisha, kuwadhulumu na kuingilia mashahidi sababu ya ushawishi wake.

Wafuasi wa Babu walikasirika ndani ya korti wakitaka aachiliwe huku wakiimba. Hakimu Bi Gandani alimwachilia kwa dhamana ya Sh500,000 au pesa taslimu Sh200,000.

Katika mahakama ya Milimani, Francis Wambugu Mureithi, aliyeshindwa na Babu Owino wa ODM anasema kwamba hakuwasilisha majibu ya kesi inayopinga uchaguzi wake katika muda unaokubalika kisheria wa siku saba.

Wafuasi wa Mbunge wa Embakasi Mashariki Paul Ongili almaarufu Babu Owino nje ya mahakama ya Kibera jana. Picha/ Evans Habil

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.