Kanisa mbioni kuwapatanisha Jubilee na Nasa

Taifa Leo - - FRONT PAGE - SILAS APOLLO na DAVID MWERE

KIONGOZI wa muungano wa upinzani, NASA, Raila Odinga amesema yuko tayari kwa mazungumzo na Jubilee kuhusu marudio ya uchaguzi wa urais, ikiwa chama hicho kitakomesha mipango yake ya kubadilisha sheria za uchaguzi.

Mnamo Jumanne, Kanisa la Kianglikana lilijitolea kupatanisha pande mbili za Jubilee na NASA, likionya kuwa vuta nikuvute kati ya pande hizo mbili inapandisha joto la kisiasa nchini.

Bw Odinga alisema mabadiliko hayo ambayo yanalenga kutekelezwa kabla ya uchaguzi huo wa Oktoba 26, ni kinyume cha Katiba.

Akiongea siku moja baada ya wabunge wa Jubilee kupitisha hoja ya kubuniwa kwa kamati teule ya kuchunguza mswada wa mageuzi hayo, Odinga alisema serikali ya Rais Uhuru Kenyatta inaongozwa na nia mbaya “kwa

kubadilisha sheria kabla ya mchezo kuisha.”

Kiongozi huyo wa NASA alikuwa katika mkutano uliotishwa na Kiongozi wa Kanisa la Kianglikana nchini (ACK) Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit ambaye aliitaka NASA kukoma kuisha maandamano bali ikumbatie mazungumzo.

Bw Odinga, ambaye alikuwa ameandamana na kinara mwenza Musalia Mudavadi, aliitaja sheria hiyo kama isiyokubalika na ambayo “inalenga kuhujumu maandalizi ya uchaguzi”.

“Hamna haya kubadili sheria wakati ambapo Mahakama ya Juu imesema kuwa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ndio ilifanya kosa. Lengo kuu ya Jubilee ni kurejesha mfumo wa kawaida wa kuwatambua wapigakura na kutuma matokeo, uliotumika kabla ya 1997. Ni makosa kwa Jubilee kubadilisha sheria wakati ambapo uchaguzi haijakamilika,” Bw Odinga akasema katika Kanisa la All Saints Cathedral.

Kabla ya kukutana na viongozi wa ACK, Bw Odinga, Mudavadi na Seneta wa Siaya James Orengo walifanya mashauriano na Balozi wa Amerika humu nchini Robert Godec na kiongozi wa ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi kutoka Muungano wa Ulaya (EU) Bi Marietje Schaake kuhusu hali ya kisiasa nchini.

Kulingana na kiongozi huyo wa upinzani mazungunzo yalihusu suala ya mabadiliko ya sheria za uchaguzi na marudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 26.

Wakati huohuo, NASA itapeleka kampeni zake katika Kaunti ya Vihiga ambayo ni ngome ya Mudavadi leo. Baadaye kesho, muungano huo utapeleka kampeni zake katika Kaunti za Busia na Kakamega.

Picha/francis Nderitu

Askofu mkuu wa kanisa la Kianglikana (ACK) Jackson Ole Sapit amsalimu kinara wa muungano wa NASA Raila Odinga aliyekuwa amewasili kwenye mkutano wa maaskofu katika kanisa la All Saints Cathedral mnamo jana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.