POLISI WANYAMA

Wavamia chuo kikuu na kuwajeruhi vibaya wanafunzi huku wakidaiwa kuwatoza baadhi yao hongo

Taifa Leo - - FRONT PAGE - Na WAANDISHI WETU

POLISI wamekashifiwa vikali kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi waliokuwa wakiandamana jijini Nairobi Alhamisi huku asasi mbili za serikali zikianzisha uchunguzi kuhusu kisa hicho.

Wanafunzi wanaodai kuathiriwa waliambia Taifa Leo jana kwamba polisi walikuwa wanataka pesa ili waache kuwashambulia.

Walisema wale waliolipa walikuwa wanasindikishwa nje ya jumba lililovamiwa, lakini waliokosa kufanya hivyo walipokea vichapo zaidi.

Polisi walipovamia hosteli za wanafunzi, inasemekana walivunja baadhi ya milango ya mbao na kujitoma ndani, na wanafunzi wengi jana walilalamika kuwa walipoteza mali yao.

“Tunaomba umma, wakiwemo wanafunzi walioathiriwa watupe taarifa za kutusaidia kuendesha uchunguzi wetu...” Afisi ya IPOA iliyo chini ya Macharia Njeru

Wengi wa waathiriwa walikuwa wanfunzi wa mwaka wa kwanza, ambao wamekuwa chuoni humo kwa chini ya majuma matatu.

Wanafunzi walioathirika zaidi ni wale waliokuwa katika upande wa barabara ya State House, darasani, kwenye maktaba, ndani ya jumba la ADD na katika hosteli. Mwanafunzi mmoja wa mwaka wa kwanza aliyefurushwa kutoka jumba hilo alisema kuwa alipigwa kwa rungu mgongoni na polisi wasiopungua 10, ambao walimtandika kitutu kwa zamu huku wamemlaza sakafuni.

“Sikulala hapo. Nililazimika kuenda Ngara na nikarudi leo asubuhi kuhudhuria mafunzo,” akasema akiongeza kuwa alilipa Sh100 kuachiliwa huru!

“Kuna wale ambao hawakuitishwa hela lakini baadhi ya wanafunzi walilazimika kulipa hela wakitoka nje ya jumba la ADD. Mimi nililipa Sh50,” akasema Clement, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza, anayesomea ramani za ujenzi.

Viongozi wa wanafunzi waliitisha kikao na wanahabari ambapo walitaka kujua jinsi polisi walivyoingia ndani ya chuo hicho.

“Kulingana na sheria zetu, maafisa wa GSU au polisi wengine hawaruhusiwi kuingia ndani ya chuo. Tunashangaa jana usimamizi wa chuo ulishirikiana na polisi kuwaruhusu kuingia chuoni na kuwanyanyasa wanafunzi,” akasema mkurugenzi wa hosteli anayeondoka Bw Ascon Kamili.

“Tunataka kuiambia serikali kuwa iwapo hawataelezea kiini cha polisi kuingia chuoni kufikia leo (jana jioni), tutafanya maandamano ya amani kutoka Kamukunji Hall 9 hadi Jumba la Vigilance tuambiwe kwa nini serikali iliamrisha wanafunzi wapigwe bila hatia,” akaongeza. Mwenyekiti wa Muungano wa Wanafunzi wa Kike chuoni humo, Bi Mary Ojwang alimtaka Waziri wa Usalama Fred Matiang’i kuomba wanafunzi msamaha kwa kuwa “yeye ndiye aliyekubali tupigwe bila hatia. Sisi si wahalifu.”

Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu (KNHRC) na Halmashauri ya kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA) zililaani ukatili huo waliotendewa wanafunzi hao ambao walikuwa wakiandama na kupinga kukamatwa kwa Mbunge wa Embakasi Mashariki Bw Babu Owino.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyumba vya habari jana, tume hiyo ilisema inachunguza kisa hicho na kuapa kuchukulia hatua maafisa waliohusika.

“Tumetamaushwa na picha zilizosambazwa mitandaoni zikionyesha polisi wakiwachapa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi kwa namna ambayo inakiuka haki za kibinadamu. Tumeanzisha uchunguzi kuhusu kisa hiki na tunatoa wito kwa umma kutoa habari ambazo zitatuwezesha kufanisha uchunguzi wetu kwa anwani; haki@knhrc.org,” ikasema taarifa hiyo.

Nayo IPOA ilisema imetuma kikosi cha maafisa wake, almaarufu Rapid Response Unit, kuchunguza suala hilo.

“Tunaomba umma, wakiwemo wanafunzi waathiriwa, watupe taarifa ambazo zitatuwezesha kuendesha uchunguzi wetu. Habari hizo zitumwe kwa anwani ya baruapepe; info@ipoa.go.ke au complaint@ipoa.go.ke,” ikasema taarifa ya afisa wa mawasiliano wa IPOA, Bw Denis Oketch. Wabunge wa mrengo wa NASA jana walisema ni makosa kwa maafisa wa polisi kuwafuata wanafunzi ndani ya kumbi za mihadhara na mabweni na kuwapiga kinyama.

“Tumetamaushwa na video zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii zikionyesha polisi wakiwapiga kinyama wanafunzi ambao walikuwa ndani ya madarasa yao. Wengine walifuatwa hadi katika mabweni yao ambapo walipigwa na kuporwa mali zao.

Tunapinga ukatili kama huu dhidi ya wanafunzi wasio na silaha,” akasema Seneta Agnes Zani kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.