Amefaidi zaidi kwa ndege kuliko wanyama

Bw Muchiri aliacha kufuga ng’ombe ili atunze aina mbalimbali za nyuni ambao wanampa faida nyingi kupitia mayai na vifaranga

Taifa Leo - - FRONT PAGE - Na DUNCAN MWERE

KABLA ya kujitosa mzimamzima kwenye ufugaji ndege wa kila aina, alifahamika na wengi kutokana na kufuga ng’ombe. Baada ya kuwaza na kuwazua alionelea ni heri kilimo cha kuku kingemzolea natija na fedha lukuki. Sasa mkulima Nixon Muchiri ni kati ya wakulima watajika wa kufuga ndege wa aina mbalimbali wakiwepo bata na kuku.mnamo mwaka wa 2000, Muchiri alianza ufugaji wa nyuni hawa japo walikuwa wachache sana lakini sasa wameongezeka zaidi.

“Nilipogura kilimo cha ng’ombe wa kisasa, nilianza kufuga kuku wakati huo wakiwa 50 na miaka kumi na sita baadaye wameongezeka na kufikia 3,000,” aeleza Muchiri katika shamba lake lililo kwenye kitongoji cha Ruthagati, viungani mwa mji wa Karatina eneobunge la Mathira Kaunti ya Nyeri.

Safari yake katika zaraa hii imekuwa ya milima na mabonde licha ya kupata ufanisi maishani. Mwaka wa 2010, alibadilisha aina za kuku wa kienyeji na kuwa na wale walioboreshwa chini ya mradi wa ‘Kienyeji Improved Chicken Institute’ unaojulikana kama KARI. Mradi huu ulikuwa na maskani katika mji wa Naivasha alikoagiza vifaranga. Baada ya kufanya vyema, alipanua kazi yake na kuagiza vifaranga kutoka jijini Kampala katika taifa jirani la Uganda. Kwa sasa Muchiri aliyeajiri wafanyakazi zaidi ya kumi na mmoja amekuwa akiagiza baadhi ya vifaranga wake kutoka kampuni ya Rainbow Roosters Chicken licha ya kutamia vifaranga kivyake.

Alidokezea Akilimali kuwa kuku wa aina hii hawakabiliwi na matatizo mengi ikilinganishwa wa kuku aliofuga hapo awali. Hii ikiwa ndio sababu kuu ana wateja chungu nzima.

“Licha ya kuwa ninajivunia tuzo la mkulima bora wa kuku katika ukanda wa Mlima Kenya kwenye maonyesho ya kilimo ya Nyeri yaliokamilika juzi katika uwanja wa Kabiruini, nina wateja kote nchini,” asema Bw Muchiri.

Anawapata wanunuzi haswa kutoka mikoa ya Nairobi, Bonde la Ufa, Magharibi na Mashariki. Vile amepata wanunuzi zaidi kupitia mitandao ya kijamii. Aidha amekuwa akitoa huduma hii kwa mahoteli na shule nyingi za eneo hili.

Pia wageni hawakosekani katika boma lake na duka lake lililo mjini Karatina linalofahamika kama Boston Chicken Centre. Bei ya kuku hutegemea umri kwa mfano bei ya kifaranga wa siku moja ni Sh100 huku wa wiki moja akiwa ni Sh150 naye wa mwezi mmoja ni Sh300. Kuku wa kike aliyekomaa ni Sh1,000 naye jogoo ni Sh1,500.

Anauza yai moja Sh30 huku kreti ikigharimu Sh900. Muchiri anaeleza kuwa yeye huuza zaidi ya vifaranga 1,000 na kuku 300 kila wiki.

Hata hivyo, mkulima huyu anawashauri wakulima wa kuku wawe waangalifu na makini kwani kuku wanahitaji kushughulikiwa kila wakati. Mojawapo ya mambo ya kimsingi wanayohitaji kuzingatiwa ni kula na kunywa ifaavyo kwa wakati.

Mahitaji mengine ni chanjo ambayo inafaa kutolewa wakati ufaao. Hitaji jingine kwa viumbe hawa ni usafi. Chumba cha kuku hao kinastahili kunadhifishwa mara mbili kwa siku.

“Mwaka wa 2013, kuku wangu waliambukizwa ugonjwa wa ‘Gumboro’ na asilimia hamsini wakafa, ni hapo nilipata funzo ya kuwachanja kwa wakati unaofaa,” aeleza Muchiri aliye na mikakati ya kuasisi chuo cha mafunzo ya ukulima.

Bw Muchiri ndiye aliyepewa jukumu la kutoa mafunzo na mawaidha kuhusu ufugaji wa kuku wa kisasa kwenye maonyesho ya kilimo ya uwanjani Kabiruini Kaunti ya Nyeri. Yeye huandaa warsha kuhusu kilimo bora cha kuku na ndege wengineo ambapo kila anayepata mafunzo haya hutozwa ada ya Sh500 kwa siku.

Mbali na kuku yeye amefuga nyuni wengine kama vile Kanga, Bata bukini, Bata mzinga, Bata, Bantans na Silky Chicken.

“Baada ya kufanya vyema, alipanua kazi yake na kuagiza vifaranga kutoka jijini Kampala katika taifa jirani la Uganda” Bw Muchiri

Picha/duncan Mwere

Baadhi ya ndege mbalimbali anaofuga Bw Nixon Muchiri kwenye shamba lake.

Mwere. Picha/ Duncan

Mkulima Nixon Muchiri akiwapa kuku chakula katika kibanda chao kwenye kijiji cha Ruthagati, Karatina eneobunge la Mathira kaunti ya Nyeri.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.