Uhuru azuru Busia akirai apigiwe kura

Amkaribisha rasmi Otuoma huku akiponda upinzani

Taifa Leo - - NEWS - AGGREY MUTAMBO na GAITANO PESSA

RAIS Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto jana walirejea katika Kaunti ya Busia kuomba kura, huku wakitumia nafasi hiyo kutetea mabadiliko tata yanayopendekezwa kwenye Sheria ya Uchaguzi.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Busia, Rais ambaye alimkaribisha rasmi aliyekuwa mbunge wa Funyula, Dkt Paul Otuoma kwenye chama chake, aliambia umati kuwa mabadiliko hayo yatazuia maafisa wa kusimamia kura katika siku zijazo kufanya dosari za kimakusudi, vinginevyo wachukuliwe hatua.

“Tunalenga kuhakikisha kuwa maafisa wanaokataa kutia saini fomu wanaadhibiwa. Kuna makosa gani kuhusu hilo?” aliuliza Rais.

Aliendelea, “Tunawataka waende jela kwa miaka mitano ikiwa watakataa kufanya kazi yao. Je, si haya ndiyo mambo ambayo wapinzani wetu walikuwa wakilalamikia? Wapinzani wangu wamenitusi kwa kusema mimi ni kifaranga cha kompyuta. Sasa tunasema usambazaji wa matokeo uwe kupitia kwa fomu ili nisiwe tena mtu wa aina hiyo.”

Wawili hao pia walitetea mafanikio yao kuhusu suala la usalama katika mkutano wa kampeni ambao ulikuwa na ulinzi mkali.

Chama cha Jubilee kimependekeza mabadiliko hayo ya sheria ambayo yameshutumiwa vikali hasa na upinzani, ukisema kuwa wanalenga kubadilisha ‘kanuni za mchezo’ ukiwa umefika muda wa mapumziko.

Viongozi hao wanalenga kuongeza idadi ya kura walizopata eneo hilo, ambazo pia zimeonekana kuongezeka tangu uchaguzi wa 2013. Katika uchaguzi wa Agosti walipata kura 35,000 kutoka 8,000 za 2013.

Bw Ruto aliwasihi wenyeji kupigia kura Jubilee akisema tayari wameanzisha miradi ya kuimarisha maisha yao. Aliorodhesha miradi hiyo kuwa hospitali ya Rufaa ya Busia, hospitali ya Kocholia, ujenzi wa barabara ya Malaba-busia, Matayos-sio Port Ring na Chuo Kikuu kina cho pe nd e k e z wacha Alupe.

“Mko tayari kwa serikali ya maendeleo ama vitendawili? Wapinzani wetu hawana ajenda. Wanazunguka tu nchi hii na mitego yao. Lakini msinaswe nayo,” alisema Bw Ruto.

“Wanafanya mchezo, wakisema hawataki uchaguzi. Uhuru Kenyatta ni amiri jeshi mkuu, lakini hana mamlaka ya kusimamisha uchaguzi, sasa wao ni kina nani watoe masharti? Nasa inastahili kuacha kudanganya wananchi.

Ikiwa hawana ajenda, wanastahili kujua uchaguzi utafanyika jinsi ulivyopangwa. Wanapanga maandamano ili tupigane kisha uchaguzi usifanyike ndipo eti mwishoe tuwe na serikali ya mseto. Hapana! Kila Mkenya, ambaye ni pamoja na wale wasio na viatu lazima wapewe nafasi ya kuchagua viongozi wao.”

Rais alikuwa amekaribishwa Busia na waziri wa Maji Eugene Wamalwa, Bw Otuoma na aliyekuwa mbunge wa Budalang’i Ababu Namwamba poamoja na waliokuwa mawaziri Chris Okemo na Fred Gumo.

Viongozi wengine walikuwa ni aliyekuwa mbunge wa Teso Kaskazini, Bw Arthur Odera.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.