Mahakama yaongezea Matiba fidia

Jaji Chacha Mwita asema fidia ya awali ilikuwa na dosari

Taifa Leo - - HABARI ZA KAUNTI - SAM KIPLAGAT na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA kuu jana ilimwongezea hadi Sh978milioni fidia ya waziri wa zamani Bw Kennedy Matiba kwa kuteswa na kusukumwa kizuizini alipokuwa akipigania kuzinduliwa kwa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa.

Jaji Chacha Mwita alimwongezea Bw Matiba kiwango hicho cha pesa baada ya wakili wake Bw John Mburu kuwasilisha ombi la kutaka kiwango cha awali cha Sh504 milioni kirekebishwe.

Alisema kulitokea makosa wakati wa kufanywa hesabu ya fidia ambayo Bw Matiba angelilipwa.

Wakili wa Serikali Bw Charles Mutinda Mutiso na Bw Mburu walifika mbele ya Jaji Mwita na kutia sahihi mkataba wa makubaliano.

“Tunaomba hii mahakama ikubali makataba wetu kwamba kiwango cha pesa ambacho Bw Matiba angelifaa kulipwa na Serikali ni Sh978 milioni na wala sio Sh504 milioni alizokuwa ameamuru Jaji Isaac Lenaola,” mawakili hao walimweleza Jaji Mwita.

Jaji Lenaola ambaye aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Juu ndiye alisikiza kesi hiyo iliyowasilishwa na Bw Matiba akiomba alipwe fidia kwa mateso aliyopata akiwa kizuizini.

Jaji Lenaola alikuwa ameagiza Serikali imlipe Bw Matiba Sh471,664,258 ikiwa ni asili mia 20 ya kiwango alichokuwa ameomba mahakama kuu imlipe kama fidia. Alikuwa ameomba mahakama imlipe zaidi ya Sh5 bilioni kwa kuzorota kwa afya yake na kubomoka kwa biashara zake akiwa kizuizini.

Kiwango kipya atakacholipwa Bw Matiba kinajumuisha Sh15 milioni kwa kuvunjiwa haki zake na Sh18 milioni za kugharamia matibabu aliyopata na anayoendelea nayo. Waziri huyo wa zamani alirudi mahakamani na kusema, “Ni jambo la busara kurekebisha hesabu ya pesa ambazo ningelilipwa kwa vile nitaendelea kupata hasara.”

Bw Matiba alikuwa mwanaspoti shupavu aliyeanzisha shirikisho la kandanda katika mataifa ya Afrika Mashariki. Alitiwa nguvuni pamoja na mwanasiasa Charles Rubia na kusukumwa kizuizini ambapo alipatwa na kiharusi cha ubongo na kukaa wiki mzima pasipo kupewa matibabu.

Alipatwa na kiharusi hicho mnamo Mei 26 1991 na kukaa bila kuhudumiwa kimatabu hadi alipopelekwa hospitali ya Nairobi hospital na kujilipia gharama ya matibabu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.