Sheria: Mashirika yapinga

Yaazimia kwenda kortini kupinga mabadiliko ya sheria za uchaguzi katika bunge

Taifa Leo - - HABARI ZA KAUNTI - Na CHARLES WASONGA

MAKUNDI ya mashirika ya kijamii yameapa kwenda kortini kupinga utekelezaji wa mabadiliko katika sheria za uchaguzi endapo wabunge wa Jubilee watayapitisha, wakisema yanakiuka Katiba.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana viongozi wa makundi hayo, chini ya mwavuli wa vuguvugu la Kura Yangu Sauti Yangu, pia walisema hawatanyamaza huku serikali ya Jubilee ikipenyeza sheria ambazo zitahujumu utendakazi wa Tume Huru Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

“Endapo serikali ya Jubilee itatumia wingi wa wabunge wake kupitisha mabadiliko haya yanayolenga kuathiri namna marudio ya uchaguzi wa urais wa Oktoba 26, basi tutawasilisha kesi mahakamani kuzipinga. Hatua hii inakwenda kinyume na katiba na uamuzi wa Mahakama ya Juu,” ikasema taarifa iliyosomwa na mwanasheria Njonjo Mue.

Bw Mue ambaye aliandamana na viongozi wengine wa vuguvugu hilo, Suba Churchil Suba, George Kegoro na Wakili Harun Ndubi alipendekeza kuwa mabadiliko kama hayo yangetekelezwa baada ya marudio ya uchaguzi wa urais ili Wakenya wapate nafasi ya kushirikishwa kikamilifu.

“Kuharakishwa kwa mabadiliko kwenye sheria ya uchaguzi kunaweza kutumbukiza taifa hili katika lindi la machafuko,” akasema.

Mswada wa mabadiliko ya sheria hizo uliwasilishwa bungeni na kiongozi wa wengi Aden Duale na kuungwa mkono ila ukakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wabunge wa upinzani.

Hata hivyo, ulishabikiwa na wabunge wa chama cha Jubilee, waliopitisha hoja ya kufupishwa kwa muda wa kuuchapisha kutoka siku 14 hadi siku moja.

Vile vile, wabunge hao walipitisha hoja ya kuundwa kwa kamati ya muda ya wabunge tisa wa Jubilee ambao wataandaa vikao vya kupokea maoni kutoka kwa umma kuhusu sheria hii. Kamati hiyo itaongozwa na Mbunge wa Baringo Kaskazini Bw William Cheptumo.

Mswada huo unalenga kupunguza mamlaka ya mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati ambapo naibu wake ataweza kutangaza matokeo ya urais andapo hatakuwepo kwa sababu moja ama nyingine.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.