Wauguzi wafurushwa makazini

Taifa Leo - - HABARI ZA KAUNTI - Na Manase Otsialo

WAUGUZI waliogoma katika Hospitali ya Kaunti ya Mandera wameamriwa kuondoka katika nyumba za serikali zilizo karibu na hospitali hiyo.

Kwenye ilani iliyowekwa katika hospitali hiyo, afisa msimamizi wa hospitali hiyo, Bw Adow Farah, amewataka wauguzi hao watafute makazi kwingineko kwa kukaidi agizo la kurejea kazini.

Bw Farah alionya kuwa wauguzi ambao watadinda kuondoka watafurushwa kwa lazima na kwa gharama yao.

“Kufuatia ilani kutoka ofisi ya waziri wa afya wa Kaunti, unatakiwa kuondoka kutoka nyumba za hospitali,” anasema ilani hiyo iliyowekwa na afisa huyo.

Pia, ameorodhesha wauguzi ambao wametambuliwa kuhusika katika mgomo huo anaodai ni haramu. “Kaunti hii iko katika mchakato wa kuwaajiri wauguzi wapya ili kurudisha shughuli za kawaida za huduma za hospitali, na unahitajika kutoa nafasi kwa kuwa hiyo ni mbinu mbadala ya kuendele na huduma za hospitali,” akasema.

Bodi ya Huduma kwa Umma ya kaunti hiyo imetangaza nafasi za ajira 257 katika idara ya afya.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.