NASA kuandamana leo afisini za UN, New York

Walenga kujuza jamii ya kimataifa kinachoendelea tangu matokeo ya kura

Taifa Leo - - HABARI ZA KAUNTI - Na CHRIS WAMALWA

WAFUASI wa Muungano wa NASA wanapanga maandamano makubwa leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York.

Waandalizi wa maandamano hayo wamesema wanalenga hatua yao ijuze jamii ya kimataifa kuhusu kinachoendelea Kenya tangu matokeo ya uchaguzi ya Agosti 8 yalipofutiliwa mbali.

Wakiongea na Taifa Leo mjini Philadelphia, Dkt George Omburo, Amos Atonga na Debra Akello, walisema matukio yanayoendelea Kenya tangu uchaguzi huo ulipofutiliwa mbali yametia hofu na jamii ya kimataifa inastahili kuiangazia nchi inapojitayarisha kurudia uchaguzi.

“Sasa hivi mnaona serikali ikiondoa ulinzi wa Bw Raila Odinga na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka, kuwahusisha Mungiki katika maandamano ya watu wasiokuwa na hatia katika barabara za Nairobi na Rais mwenyewe akishtumu na kujaribu kuhujumu Idara ya Mahakama kwa kuwa uamuzi haukumpendelea,” walisema kupitia kwa taarifa yao.

Iliendelea, “Hali ya Kenya tunavyoongea sasa ni taharuki. Na ndiyo sababu tuna matukio hayo Jumamosi hii New York na New Jersey ili masuala haya yaweze kutambulila, huku tukisherehekea uamuzi wa kihistoria ambao umefanya Kenya kuwa kielelezo cha demokrasia Afrika.”

Maandamano hayo yataanza saa tano asubuhi na kumalizika mchana kwa mkutano wa wanahabari.

Baada ya New York, walisema kuwa wataelekea New Jersey kwa mkutano mwingine, ambao pia utatumika kuchangashia pesa kampeni za muungano wa NASA.

Wakati huohuo, wafuasi hao wa NASA wameitaka serikali iwarejeshee Bw Odinga na Bw Musyoka walinzi wao.

Katika taarifa yao, wafuasi hao waliopo Amerika na Canada walisema ikiwa jambo lolote litamfika kiongozi huyo wa upinzani, utawala wa rais Kenyatta utahitajika kujibu.

“Mgombea wa urais ni rais anayesubiri kuingia mamlakani na anastahili kulindwa. Hii ndiyo sababu wafuasi wa NASA Amerika wanashtumu vikali hatua ya utawala wa Jubilee kuwaondoa walinzi wa mgombea wa urais anayeongoza, Bw Odinga na mgombea mwenza Musyoka.” ikasema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Bw Jack Ambuka wa New Jersey ilieleza.

Viongozi hao wawili walinyang’anywa walinzi wao Jumatatu jioni. Maafisa hao kutoka kwa kitengo cha General Service Unit, walirudishwa kwa makao makuu Nairobi, mkesha wa siku ambapo maandamano yalipangwa kufanyika dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.