ERC yaadhibu vituo 19 kwa kuyauzia magari mafuta chafu

Taifa Leo - - HABARI ZA KAUNTI - Na FAUSTINE NGILA

TUME ya Kawi (ERC), jana ilifunga vituo kadha vya kuuza mafuta na kutoza vingine faini kwa kuuza mafuta chafu yanayohatarisha injini za magari nchini.

Takriban vituo 19 vilipatikana na hatia ya kuuza mafuta chafu wakati wa msako wa tume hiyo.

Kaunti ya Siaya inaongoza kwa uuzaji wa mafuta bandia kwa vituo vinne, ikifuatwa na Busia (2) na Nandi (2). Kaunti za Nairobi, Mombasa , Kisumu, Kilifi, Homa Bay, Trans Nzoia, Vihiga, Nakuru, Kiambu na Murang’a zilipatikana na kituo kimoja kila moja chenye mafuta chafu.

Baada ya kufanya uchunguzi wake katika vituo 753 vya mafuta katika kipindi kilichoanza Julai hadi Septemba mwaka huu, tume hiyo ilipata baadhi ya vituo vimekuwa vikifanya makosa manne.

Kwenye taarifa ya tume hiyo katika tangazo lililochapishwa gazetini jana, vituo hivyo vilinaswa vikiuza mafuta ya Dizeli yaliyochanganywa na mafuta taa (vituo 13), Petroli iliyochanganywa na mafuta taa (vituo 10), Petroli ya kuuzwa katika masoko ya kigeni (vituo 3), na Dizeli ya kuuzwa katika masoko ya kigeni (vituo 3).

Mwezi Septemba umeshuhudia zaidi mafuta chafu yakiuzwa kwani katika ya vituo hivyo 19, 9 vilinaswa mwezi huu.

Ni vituo 3 pekee vilinaswa mwezi Agosti, hasa kutokana na uchaguzi mkuu, huku vituo 6 vikifumaniwa Julai vikiendesha biashara hiyo haramu.

Vituo vyote vilipigwa faini ya kati ya Sh89,000 na Sh500,000 huku vituo sita vilivyolemewa kujaza mafuta safi vikifungwa na tume hiyo ili kuwalinda wenye magari.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.