15 wafariki kutokana na mkurupuko wa malaria

Taifa Leo - - HABARI ZA KAUNTI - Na KEN BETT

WATU 15 wameaga dunia kutokana na mkurupuko wa malaria katika wilaya ya North Horr, Kaunti ya Marsabit kwa muda wa wiki moja iliyopita.

Kwa mujibu wa ripoti iliyowasilishwa katika bunge la kaunti hiyo na wawakilishi wadi za Dukana, Illeret na North Horr, miongoni ya waliyoaga dunia ni pamoja na watoto watatu.

Watu wawili waliaga dunia katika wadi ya Illeret, kumi Dukana na wengine watatu North Horr.

Afisa mkuu wa Shirika la msalaba mwekundi wa kaunti hiyo Talazo chucha, amethibitisha maafa hayo na kuahidi kushirikiana na serikali ya kaunti kuwatuma wauguzi 60 ili kukabiliana na janga hilo.

Bi Talaso alitaja mgomo wa wauguzi na ukosefu wa dawa kama changamoto kubwa ya kukabiliana na mkurupuko huo.

Katika mkutano ulioandaliwa katika afisi ya Gavana Mohammud Ali, mkurugenzi mkuu wa huduma za afya Dkt Boru Okotu alidokeza kuwa kati ya watu 186 waliochunguzwa na watu 136 walipatikana na dalili za ugonjwa huo.

Bw Okotu alihoji baadhi ya lalama kutoka kwa wagonjwa ni pamoja na kuhisi joto jingi, kuumwa na kichwa, kutapika, maumivu ya mgongo, kuendesha damu na kutapika mara kwa mara.

Idadi kubwa ya waliyoathirika ni kutoka maeneo ya mashinani ambao hawawezi kufikia vituo vya huduma ya afya kwa haraka.

Vijiji vilivyoathirika zaidi ni pamoja na Konye, Kubi Adi, Diid Gola, Garwole na Daka Baricha.

Maeneo mengine ni Barambate, Kubi Adi, Konon-gosi, El-beso na Malabot.

Mwakilishi wa wadi wa North Horr Tura Ruru alidokeza kuwa ameweza kugharamikia malipo ya hospitali ya watu 13 kupokea matibabu kutokana na mkurupuko huyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.