Madaktari sasa kuvuna figo za wafu

Wizara ya Afya inafanya mashauriano kufanikisha sheria

Taifa Leo - - HABARI ZA KAUNTI - Na WINNIE ATIENO

MADAKTARI nchini sasa wataanza kuvuna figo kwa wafu ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaougua maradhi sugu na hatari ya figo endapo watapata idhini kutoka kwa familia za marehemu.

Aidha, kulingana na madaktari, wagonjwa ambao wanachungulia kaburi au mahututi ambao hakuna njia ya kuokoa maisha yao pia wanaweza kutolewa figo zao iwapo familia zao zinakubali.

Mwenyekiti wa Muungano wa Kamati ya Madaktari wa Figo nchini Dkt Maranga Wambugu alisema wizara ya afya inaendelea kufanya mazungumzo na wawekezaji kadha ili kufanikisha sheria za kupandikiza figo za ‘wafu’.

Mwezi Juni mwaka huu, Rais Uhuru Kenyatta alipitisha mswada ambao utarahisisha Wakenya kutoa msaada wa figo zao kwa upandikizaji na utafiti.

Barani Afrika, Afrika Kusini ndio nchi inayotumia teknolojia hiyo ya kupandikiza figo kwa wagonjwa, akaongeza, Dkt Wambugu.

Figo hung’olewa kwa wagonjwa hao ambao hawana tamaa yakupona kwa idhini ya jamaa zao na kupandikizwa kwa wagonjwa wanaouguza maradhi ya figo.

Prof David Harris kutoka chuo kikuu cha Sydney aliwarai Wakenya kukumbatia utabibu wa maradhi ya figo kwa kupandikiza figo za wafu badala ya kusafisha figo zao kwa mbinu ya ‘dialysis’.

“Tutawasaidia kwa kuwapa mafunzo ya kisasa kwa wahudumu wa afya wakiwemo madaktari na wauguzi ili wapeana matibabu ya figo. Ninawapa changamoto muanze kuchangamkia suala hilo ili Kenya iwe kielelezo duniani kwa mataifa mengine,” said Prof Harris.

Dkt Wambugu alisema maisha ya mgonjwa ambaye amepewa figo mpya huimarika zaidi kuliko yule ambaye huenda kufanyiwa matibabu ya kuoshwa figo.

Aliwataka Wakenya kupeana figo zao kwa wanaohitaji.

“Mpango huo utasaidia Wakenya wengi ambao wanateseka,” akasema.

Wakiongea kwenye hoteli ya Pride Inn Paradise huko Mombasa kwenye warsha yao, Dkt Wambugu alisema mgonjwa ‘aliyekufa’ na anataka kupeana figo yake atathibitishwa na madaktari maalum.

Naye Waziri wa Afya Cleopa Mailu alionya kuwa Wakenya milioni nne wanauguza maradhi ya figo huku wengi wakiwa na hatari ya figo zao kukosa kufanya kazi.

“Takriban watu 10, 000 wanahitaji kuoshwa figo (dialysis) lakini inasikitisha kuwa asilimia 10 pekee ndio wanaopata huduma hizo kutokana na uhaba wa wataalam wa afya katika sekta ya afya kwenye hospitali za umma,” akasema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.