Polo mlevi apiga nduru baada ya chokoraa kumuibia dozi

Taifa Leo - - DONDOO! - Na John Musyoki

SINEMA ya bure ilishuhudiwa mjini hapa kalameni alipopiga nduru akilia baada ya kupokonywa chupa ya pombe na vijana wanaorandaranda mtaani.

Inasemekana jamaa alikuwa na mazoea ya kutembea mtaani huku akinywa pombe yake badala ya kumalizia dozi klabuni.

“Alikuwa akidharau watu sana hasa vijana hao wa mtaani,” alisema mdokezi.

Duru zinasema mara nyingi kalameni alikuwa akirushia watu cheche za matusi na kuwaambia kuwa hawakuwa na pesa za kununua kileo kama yeye kwani alikuwa bwanyenye.

Tabia ya kuringia watu kwa pombe ilimfanya kujuta vijana wa mtaani walipomnyemelea unyo kwa unyo na kumnyang’anya pombe yake na wakatimua mbio. Yasemekana baada ya jombi kupokonywa dozi na vijana hao kupotelea vichochoroni, aliangua kilio.

Jamaa alianza kupiga nduru lakini watu walimpuuza hasa waliomfahamu. Kalameni alizidi kubahatisha iwapo angepata vijana hao lakini juhudi zake zilionekana kuambulia patupu kwa sababu walikuwa wametoweka kabisa.

Haikujulikana iwapo kalameni alituliza moyo na kurudi klabuni kununua pombe nyingine na kuiteremsha.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.