Jubilee yajichimbia kaburi kubadili sheria za uchaguzi

Wanasiasa wanaoegemea JP wana hakika gani kuwa watadumu serikalini?

Taifa Leo - - BARUA - Na DOUGLAS MUTUA

WASEMAO husema mchimba kisima huingia mtuwe au mwenyewe. Ikiwa, kama mzalendo wa Kenya, unatafuta ithibati kwamba chama tawala cha Jubilee kinajihini, tazama mambo yanavyoendelea kwa jirani yetu Uganda.

Dikteta wa miaka mingi kwa jina Yoweri Kaguta Museveni amewashawishi wabunge wake walio wengi kubadilisha sheria inayomzuia mkongwe yeyote wa miaka zaidi ya 75 kuwania urais.

Museveni mwenyewe ana umri wa miaka 73 na hivyo basi sheria isipobadilishwa hawezi kutafuta kipindi cha sita – rudia sita – ifikapo mwaka wa 2021.

Hilo halinikoseshi usingizi kamwe kwa maana Museveni amejulikana kwa kuua wapinzani wake tangu anyakue uongozi kwa maasi mnamo 1986, seuze kukicharura kijikaratasi cha Katiba?

Unaonizuga akili ni utando wa kiburi katika Jubilee nchini Kenya ambao kawaida huwazingira watu wakipata mamlaka ukawapofusha wasione historia inavyojirudia.

Museveni alibadilisha sheria akinuia kumzima mkongwe Dkt Milton Obote. Zama hizo Museveni hakutafakari kuhusu uzee wake mwenyewe.

Dkt Obote alifuata njia ya marahaba, naye Museveni sasa amekonga na kisu alichokinoa mwenyewe kinamtishia kwa makali.

Maumbile yana jinsi ya kuwalipizia kisasi wanyonge dhidi ya watesi. Ni kwa mintaarafu hii ambapo – japo sikubaliani na mambo mengi yanayoendelea katika Mahakama ya Juu nchini Kenya – napinga njama za kutunga sheria kuiadhibu.

Huenda jitihada za Jubilee katika Bunge la sasa kutunga sheria ili kuwakomesha Jaji Mkuu David Maraga na wenzake zikawadhuru waasisi wazo siku zijazo.

Si siri kwamba Bw Maraga na baadhi ya majaji katika Mahakama hiyo wanachukiwa hadi ya kuchukiwa na Rais Uhuru Kenyatta na kundi lake kwa tuhuma kwamba walikula njama wakabatilisha ushindi wao katika Uchaguzi wa urais wa Agosti 8, 2017.

Na ni siri iliyo wazi kwamba sheria inayopendekezwa na wabunge wa Jubilee walio wengi ni mkuki unaolenga kumwangamiza Maraga na wenzake.

Swali kuu hapa ni, wingi wa wabunge wa Jubilee ukiwawezesha kuwang’oa majaji wa sasa au hata kubadilisha jinsi uchaguzi unavyofanywa, sheria hiyo itatumika dhidi ya nani usoni?

Tunaweza pia kujiuliza: Rais Kenyatta na kundi lake wana hakika gani kwamba watadumisha wingi wao katika chaguzi zote kuu zitakazofanyika usoni?

Endapo njama hiyo itafanikiwa, basi mustakabali wa nchi hii kisiasa utaingia katika hali taabani si haba.

Si kutokana na sheria hiyo pekee bali pia kwa kusadikisha wanasiasa kwamba wanaweza kubadili sheria kiholela ziwafae binafsi, badala ya kwa ajili ya manufaa ya nchi nzima.

Wanasiasa wanaoegemea siasa na itikadi sampuli ya hizo za Jubilee wana hakika gani kuwa wao pekee ndio watakaodumu serikalini; hawatajipata katika upinzani siku moja?

Watahisi vipi kiburi na ujeuri ukitumiwa kuwakandamiza, tena wakumbushwe kwamba mateso watakayopitia ni kutokana na uchache wao?

Kubadili sheria zikufae wakati huu ni sawa na kujichimbia kaburi bila kujua, likakaa wazi likisubiri siku yako ya kuingia humo kama mfu.

Tukumbuke mwendelezo wa sera za dhuluma alizowafanyia watu mwendazake Jomo Kenyatta ziliwadhuru zaidi waliokuwa wake alipofariki na mrithi wake, Daniel Moi, akaamua kufuata nyayo za marehemu. mutua_muema@yahoo.com

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.