Mbona serikali haina mikakati kukabili uhaba wa chakula?

Taifa Leo - - BARUA - Na CHARLES WASONGA

MAJUZI serikali ilisema kuwa inatarajia mavuno ya mahindi mwaka huu kupungua kwa asilimia 20 kutokana na changamoto zilizowakabili wakulima katika maeneo kunakokuzwa zao hilo kwa wingi.

Wizara ya Kilimo ilitaja changamoto hizo kuwa uvamizi wa viwavi na uhaba wa mvua ya kutosha hasa katika maeneo ya kaskazini mwa Rift Valley. Hali hiyo ilisababisha kuharibika kwa mimea ya mahindi katika zaidi ya ekari 40,000 za mashamba katika eneo hilo ambalo huchukuliwa kuwa ghala kitaifa la zao hilo .

Kwa hivyo, inakadiriwa kuwa ni magunia 35 milioni ya mahindi yanayotarajiwa kuvunwa kote nchini katika msimu wa mavuno unaoanza Oktoba mwaka huu, ilhali ni magunia 42 milioni yaliyotarajiwa kuvunwa mwaka huu.

Hii ina maana kuwa huenda baa la njaa likashuhudiwa nchini kwa mara nyingine kuanzia mwishoni mwa mwaka huu na mapema hapo mwakani. Wakati huu takwimu zinaonyesha kuwa takriban Wakenya 2.8 milioni wanakabiliwa na hatari ya kuathiriwa na makali ya njaa.

Lakini kinachoshangaza ni kwamba hamna dalili zozote kwamba serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na hali hii iliyoipelekea kuazisha mpango wa kuagiza mahindi kutoka nje kwa bei ya juu.

Mahindi hayo yaliuziwa wasagaji kwa bei ya Sh2,300 licha ya kununuliwa kwa Sh3,600 kutoka mataifa nje kama vile Mexico. Ni chini mpango huo ambapo bei ya unga ilipunguzwa kutoka Sh180 hadi Sh90 kwa paketi moja ya kilo tangu Julai mwaka huu.

Mapema mwezi huu, serikali ilitangaza kwamba itanunua mahindi kwa bei ya Sh3,000 kwa gunia, katika msimu huu wa mavuno. Lakini wakulima wamepinga bei hiyo wakidai kuwa ni duni na haitawawezesha kufidia gharama ya uzalishaji zao hilo. Wanataka bei hiyo iongezwe hadi kufikia angalau Sh3,600.

Kwa maoni yangu, pendekezo hilo la wakulima, haswa, wa North Rift linafaa zaidi kwa sababu mojawapo ya sababu iliyopelekea kupanda kwa bei ya unga wa mahindi mwaka huu ilikuwa ni ukosefu wa mahindi katika maghala ya Bodi ya Nafaka na Mazao (NCPB) kote nchini.

Itakuwa aibu kwa serikali kuanza kuagiza mahindi kutoka nje kwa bei ya juu mwaka ujao, ilhali ina nafasi ya kutenga pesa za kutosha kununua mahindi kutoka kwa wakulima wa humu nchini.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.