Aibu kuu timu ya taifa kukaa gizani

Taifa Leo - - BARUA -

Inashangaza na kuvunja moyo kuona timu zetu za taifa za voliboli zikiendelea kuhangaika zinapojiandaa kupeperusha bendera ya Kenya katika mashindano ya Afrika mwezi ujao. Ripoti kuwa timu hizo zinafanya mazoezi katika ukumbi wa kimataifa wa Kasarani bila stima na maji ni ‘dhihaka’ kwa Wakenya hasa baada ya nchi kuunda Halmashauri ya Kusimamia Viwanja nchini (Sport Kenya).

Katika sheria za Kenya za michezo za mwaka 2013, halmashauri hiyo ilipewa karibu majukumu 20 yakiwemo kufanikisha maandalizi ya timu za taifa kushiriki mashindano ya kimataifa.

Kazi yake nyingine ni kuweka vifaa vya michezo katika hali nzuri. Inakuwaje kwamba timu ya taifa kama Malkia Strikers ama yoyote ile inafanya mazoezi katika ukumbi uliojaa giza, miaka 53 baada ya kuwa mwanachama wa Shirikisho la Voliboli duniani (FIVB)?

Sport Kenya inafaa kuhakikisha taa katika ukumbi wa Kasarani zinafanya kazi mbali na kuwepo mwanga wa kutosha kuwezesha timu kufanyia mazoezi bila bughudha yoyote.

Haifai kabisa timu za taifa kuhangaika kila mara inapotumia vifaa vya umma kama Kasarani.

Itakumbukwa kuwa mojawapo ya majukumu ya Sport Kenya ni kuimarisha utalii kupitia michezo. Timu za taifa za michezo ikiwemo ya voliboli hutekeleza jukumu hili la kuvumisha nchi hii kule nje bila malipo, hivyo basi hamna mantiki ya kufanya mazoezi katika mazingira kama yale ya Kasarani.

Mashindano ya voliboli ya Afrika ya wanawake yatafanyika Oktoba 7-14 jijini Yaounde nchini Cameroon, huku yale ya wanaume yakiandaliwa Oktoba 22-29 jijini Cairo nchini Misri.

Ni mashindano yanayofaa kuchukuliwa kwa uzingativu unaofaa. Yote mawili ni ya kufuzu kushiriki mashindano ya dunia ya wanaume yatakayofanyika Septemba 10-30 mwaka 2018 nchini Bulgaria na Italia nayo ya wanawake yakiandaliwa Septemba 29 hadi Oktoba 20 mwaka 2018 nchini Japan.

Malkia Strikers ni mabingwa mara tisa wa Afrika na wameshiriki pia Olimpiki, All-africa, mashindano ya dunia, Kombe la Dunia na yale ya Grand Prix. Wanaume wa Kenya watakuwa mawindoni kusaka tiketi ya kufika ulingo wa dunia kwa mara ya kwanza kabisa.

Kutokana na umuhimu mkubwa wa mashindano ya Afrika, maombi yetu ni kuwa serikali, Sport Kenya na Wizara ya Michezo zichukue hatua za haraka kurekebisha mazingira ya mazoezi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.